Wadau wa sheria watakiwa kutenda haki kwenye kutoa maamuzi

Baadhi ya wanachama wa TAMWA mkoa wa Arusha.
Mkuu wa wilaya ya Arusha Said Mtanda akipata maelezo kwenye Banda la TAMWA Jijini Arusha.

 Na Mwandishi Wetu, Arusha


Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda ametoa rai kwa wadau wa sheria wakiwemo mahakimu kuhakikisha wanatoa haki kwa wadau wa mahakamani ili wawe na imani katika kutatua kesi zinazofikishwa mahakamani.


Aidha ameagiza wanasheria kutumia zaidi siku ya wiki ya sheria ili kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi inayoongoza katika Wilaya na Mkoa wa Arusha.


Mtanda aliyasema hayo leo Jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa wiki ya sheria  yenye kauli mbiu isemayo "Zama za Mapinduzi ya nne ya Viwanda, Safari ya Maboresho kuelekea Mahakama Mtandao" kushirikisha wadau mbalimbali wa sheria kikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Nchini Tanzania (TAMWA) pamoja na Halmashauri ya Jiji la Arusha.


Amesema baadhi ya mahakimu wanatumia fursa za kujipatia fedha kupitia kesi mbalimbali na hatimaye wananchi kukosa haki na wengine haki zao kucheleweshwa wakiwa mahabusu.


Amesema ni vema watoa haki wakaepuka rushwa na kutenda haki ili wadau wa mahakamani wawe na imani na mahakama katika utoaji haki na si ucheleweshwaji.


"Arusha kuna migogoro  mingi ya ardhi hivyo jaribuni kuitatua ikiwemo kuhakikisha mnatoa haki bila upendeleo na msiwacheleweshe wanaotaka haki kupata haki zao" alisema Mkuu wa wilaya.

 

Pamoja na mambo mengine alipongeza wadau wa Haki ikiwemo TAMWA kushiriki katika wiki ya sheria inayoratibiwa na Mahakama na kuwataka kuelezea uhalisia wa ukiukwaji haki za binadamu wanaokutana nao ili kuweza kufanyiwa kazi .


"Nimefurahi kuwaona kwenye Banda hili nawapongeza  sana TAMWA na Jiji la Arusha kuungana na Mahakama kutoa elimu kwa wananchi" Alipongeza Mkuu wa wilaya na kuongeza.


"Mnafanya vizuri kutetea wanawake na watoto endeleeni kutoa elimu zaidi na halamshauri ya Jiji endeleeni kutoa elimu mbalimbali katika wiki hii ya sheria ili wananchi wajue kuhusu migogoro wanayokumbana nayo wanawake na watoto" alisema Mtanda


Naye Jaji Mfawidhi Kanda ya Arusha, Mosses Mzuna amesema kupitia mahakama mtandao mwaka huu wa 2022 wameshasajili kesi 56 na wanaishukuru serikali kwa kujenga majengo mazuri ya mahakama yanayotoa huduma za kisheria kwa pamoja.


Wakati huo huo, Mwanasheria wa Jiji la Arusha, Iddi Ndabhona akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha alisema Jiji la Arusha linaendelea kutoa msaada wa kisheria katika maeneo mbalimbali  ya Jiji la Arusha migogoro  hiyo ikiwa ni pamoja ardhi na mirathi kwani wanawake wengi na watoto wanashindwa kumiliki ardhi au mali wanazoachiwa na Wanaume zao pindi wanapofariki  kwa sababu ya baadhi ya mila kandamizi kwenye jamii zao. 


Ashura Mohamed ni mwanachama wa TAMWA akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa TAMWA Rose Ruben amesema kuwa TAMWA wako mstari wa mbele katika kutetea wanawake na watoto kwamba wameshiriki wiki ya Mahakama kwa lengo la kuelezea mamlaka husika namna wanawake na watoto wanavyofanyiwa ukatili kwenye jamii zao.


"TAMWA tutaendelea kupaza sauti ili kudhibiti ukatili kwa wanawake na watoto kupitia wiki hiyo ya sheria na lengo letu nikuona vitendo vya ukatili vimekoma” amesema Ashura .


Wiki ya Sheria inayoratibiwa na Mahakama imeanza na elimu inatolewa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha ikiwemo eneo la TBA lililopo Jirani na Makumbusho ya Jiji la Arusha.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post