UNAIDS na NACOPHA watoa elimu ya ukatili, unyanyapaa, *Elimu duni miongoni mwa jamii yasababisha ongezeko la matukio hayo

Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Arusha A Dc Angela Mvaa aliyevaa miwani akizungumza wakati wa mafunzo ya ukatili,unyanyapaa na uviko kwa wajumbe wa Kiwawara 


Na Seif Mangwangi, Arusha

IMEELEZWA kuwa matukio ya mauaji na ukatili ikiwemo unyanyapaa wa watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, unyanyasaji wa kijinsia kama ubakaji na kulawiti yameendelea kukua nchini kutokana na elimu duni miongoni mwa jamii.


Mwenyekiti wa kikundi cha wanaume wanaoishi nna VVU Arusha Alex Ikera akizungumza na waandishi wa habari
 
Akizungumza na wanachama wa Kikundi cha wanaume wanaoishi na virusi vya Ukimwi Arusha (Kiwawa), ambao pia ni wanachama wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na VVU, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Arusha Angela Mvaa amesema Elimu zaidi inatakiwa kutolewa ili watu wajue madhara ya kuficha matukio ya unyanyasaji wa kijinsia, ambayo yamekuwa yakitokea katika ngazi ya jamii nchini.


 Amesema kutokana na kukosa elimu na kujua mahali ambapo wataweza kuripoti matukio ya namna hiyo baadhi ya matukio yamekuwa yakiishia ngazi ya familia na matokeo yake ni kuendelea kukua kwa vitendo hivyo vya kikatili kwenye jamii.


"Utakuta familia inapata tatizo, miongoni mwa wanajamii wanaogopa kutoa taarifa, familia inaamua kuyamaliza, huku  aliyeathirika akawa hajaridhika na hivyo kuendelea kuumia na kuathirika kisaikolojia, ili suala la unyanyapaa na ukatili viishe ni  lazima vyombo vya kisheria vifanye kazi yake," Amesema.


Wakichangia mada katika mjadala huo, baadhi ya wajumbe wa baraza wamesema wamekuwa wakishindwa kuripoti matukio ya unyanyasaji kutokana na kutokutambulishwa kwa viongozi ngazi ya jamii kama Mwenyekiti wa kijiji au Balozi.


"Sisi kama watetezi tumekuwa tukipata hofu ya kuripoti matukio haya kwa watendaji wa Kiserikali, kwa kuwa hatujatambulishwa   kwenye jamii kwa hiyo tunaomba tukutanishwe aidha na balozi au hata mwenyekiti wa kijiji, ili tusije kuonekana ni wachochezi kwa kutaka kwenda mbele zaidi kisheria,"wamesema.


Amina Mollel ambaye anaishi na virusi vya VVU kwa zaidi ya miaka kumi sasa, anasema ili kupunguza tatizo la unyanyapaa na ukatili wa kijinsia kila mmoja anapaswa kujua nafasi yake katika jamii na kuonyesha huruma kwa wengine.


"Mfano kuna jirani yetu mtoto wake mdogo aliwahi kubakwa  na kijana kidato cha pili, yule mama aliona aibu kwenda polisi aliogopa mtoto wake kudhalilika, akaficha huku wazazi wa mtoto  aliyebaka wakamhamisha mtoto wao kwa kumpeleka kijijini kusoma na hivyo kesi kuisha hivyo hivyo,"anasema na kuongeza:


"Miaka mitatu iliyopita kuna Mtoto wa darasa la kwanza alibakwa na Baba yake mzazi na kumwambukiza VVU, nilijitolea kumsaidia Mama wa Mtoto  kwenda polisi na kufungua kesi, mpelelezi alitoa maagizo mama amkamate mumewe, ampeleke polisi, lakini ilishindikana sababu mtuhumiwa alikuwa anaingia usiku na kutoka alfajiri, lakini kama vyombo vya kiserikali vingekuwa makini huyu mtuhumiwa leo hii angekamatwa,"Anasema.Angela Mvaa, Afisa maendeleo ya jamii Halmashauri ya Arusha anawataka wajumbe wa Baraza hilo kuchukua mawasiliano ya viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, kata, polisi, ofisi ya ustawi wa jamii, polisi dawati la jinsia, maafisa Maendeleo ya jamii na hata mkurugenzi na kuripoti taarifa zozote za unyanyasaji.


"sisi tukipigiwa simu tunafika haraka eneo la tukio na muathirika anapelekwa polisi na hospitali mapema sana, tunaomba asasi mtusaidie, na kama mtu yuko karibu pale hospitali ya Mount Meru kuna kitengo mtapewa misaada wa haraka,"Amesema Angela.


"Serikali imekuwa na  njia mbalimbali kuhakikisha inapata taarifa sahihi na ni nani mtu sahihi wa kumpatia taarifa, kwa hivi sasa tumepata mafanikio sababu tunahakikisha ngazi zote tunapata taarifa ikiwemo mwanasheria, afisa maendeleo ya jamii lakini pia kuna watoto mashuleni wamejengewa uwezo tunawatambua kama 'vinara' wa kutambua na kupokea taarifa za ukatili na kuziripoti ngazi za juu. pia wapo bodaboda na wenyewe wanafanya hizo kazi. tumejikita sana maeneo ya vijijini, mfano mzuri Halmashauri ya Arusha Dc kata ya Musa,"Amesema.


Pia anasema kama familia tukisimama vizuri watoto watajua dhana ya ukatili na ukatili itatokomezwa kwa ngazi zote na kutolea mifano ya ukatili kwa ni pamoja na  ukeketaji,, kunyima mtoto asiende shule ni ukatili.


Alex Ikera Mwenyekiti wa Baraza la watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi Konga Arusha, anasema ukatili upo lakini unyanyapaa na ubaguzi, kwa wanaoishi na VVU ni mkubwa.


"Hata hivyo tunashukuru shirika la umoja wa Mtaifa la UNAIDS kwa kushirikiana na Nacopher kutuwezesha kufanya mafunzo ya unyanyapaa na Uviko, sisi kama baraza tunafarijika kupata misaada huu kusaidia jamii,"Anasema Ikera ambaye pia amekuwa akiishi na maambukizi ya VVU tangu mwaka 1995.


Anasema unyanyapaa na ubaguzi ni matukio yaliyokuwepo  sana hapo nyuma lakini yanaaelekea kuisha, " tunajitahidi kutoa elimu ili kupunguza, baada ya watu kupata elimu, awali watu walikuwa wanaenda mbali kuchukua dawa za kufubaza makali ya HIV sasa hivi ni tofauti, tatizo watu walikuwa wanagopa kuonana na wenzao katika kituo kimoja, hasa majirani,"anasema."Mimi naishi na maambukizi ya VVU kuanzia 1995 siri ya kwanza ni kukubaliana na hali yako, ondoa fikra kwamba unaumwa, mke wangu alikufa mwaka 1999, kwa ugonjwa wa malaria na baadae tulifanya uchunguzi na kugundua alikuwa nayo,"anasema. 


Ikera anasema kupitia mradi huo wa UNAIDS wameweza kuhamasisha zaidi ya watu 2000 kupata chanjo ya Uviko-19.


Kwa upande wake Amina Mollel anashukuru UNAids kwa mafunzo ya kijinsia na ukatili dhidi ya waathirika wa VVU lakini pia jamii nzima na kwamba miradi huo umewasaidia kuweza kuibua na kuripoti matukio ya kikatili ambayo yamekuwa yakiendelea katika jamii.


Francis Temu ambaye ni mjumbe wa kikundi cha wanaume wanaoishi na virusi vya Ukimwi  (Kiwawara) Arusha,  na mwenyekiti mstaafu wa kikundi hicho anasema katika mafunzo hayo wameweza kuzungumzia ukatili wa kijinsia na kwamba mafunzo hayo yatawasaidia kueneza elimu kwa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia kama ulawiti na ubakaji, ukatili wa kisaikolojia, kipigo n.k. lakini pia kutoa taarifa kwa wakati kwenye vyombo vya kisheria na mtuhumiwa kukamatwa.


" Kuna shida kubwa kwa wanaume kuhusu kujua afya zao, wengi wanafikiri mke akishapima basi na yeye tayari ni mzima, tunawashauri waende wakapime ili wapate uhakika kamili wa afya zao, lakini pia waache michepuko,"amesema.


Kwa upande wake Meneja ushirikishwaji sekta binafsi na jamii Methew Kawogo kutoka Baraza la Taifa la watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (Nacopha), anasema baraza hilo la Taifa la watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, kwa kuwezeshwa na shirika la UNAIDS limeweza kutoa mafunzo ya ukatili wa kijinsia, unyanyapaa na ubaguzi na Uviko-19. 


Anasema shirika limeweza kufikia makundi hatarishi kama Dada Poa, madereva wa magari makubwa, bodaboda, na wavuvi.


"Nacopha kupitia mradi huu imeweza kufikia mikoa mitano Tanzania bara ya Arusha, Shinyanga, Mara, Pwani na Mwanza ambapo tumekuwa tukishirikiana na viongozi na watendaji ngazi ya Mkoa na Wilaya katika kufikisha ujumbe kwenye jamii," amesema Methew.
This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post