*Asema Flattey alipatwa na msongo wa mawazo kukimbilia ACT
Na Seif Mangwangi, APC TV Arusha
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), bara, Stephen Wassira amesema ameshavunja makundi ndani ya Chama hicho katika mikoa ya Arusha na Manyara na kuwataka waliokuwa wabunge kujitokeza kuwanadi wagombea waliopitishwa na Chama ili kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu 2025.
Aidha amewataka wabunge hao ambao hawakuteuliwa na Chama kujua kwamba nafasi ya ubunge sio kazi ya kudumu (Permanent job), lakini ndani ya chama bado kuna nafasi nyingi za kuteuliwa na wakaendelea kutekeleza majukumu mengine tofauti na ubunge.
Akizungumza Jana Septemba 4,2025 katika kikao na waandishi wa habari amesema anaamini aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo ambaye jina lake halikurudishwa na kamati kuu ya CCM atakuwepo kwenye kampeni za kumnadi aliyekuwa hasimu wake Paul Makonda na Dkt Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya Urais.
Amesema katika ziara yake ya Mkoa wa Arusha na Manyara hususan katika majimbo ya Arusha Mjini na Mbulu Kwa nyakati tofauti aliweza kukutana na viongozi wote wa CCM waliohusika kuwapigia kura wagombea walioteuliwa na Chama hichona kukubaliana kuvunja makundi ijapokuwa katika Jimbo la Arusha, Mrisho Gambo hakuwepo kwenye kikao.
“Nilifanya kikao na viongozi wote wa Jimbo la Arusha na Mkuu wa Mkoa kama kamisaa wetu ndani ya Serikali pia alikuwepo, tukakubaliana kuvunja makundi yote, Gambo hakuwepo lakini naamini atakuwepo kwenye kampeni zetu, yeye bado ni mwana CCM tena mzoefu na anaweza kuteuliwa Kwa nafasi zingine tena za juu,”amesema na kuongeza:
“Hata pale Mbulu tulikutana na viongozi wote na waliogombea akiwemo Flattey Maasay ambaye baada ya mazungumzo alisema aliamua kwenda upinzani baada ya kupatwa na msongo wa mawazo lakini nilipomfanyia counselling akaelewa na kuamua kurudi nyumbani na tumekubaliana atatembea Mkoa mzima kuwanadi wabunge, madiwani na Rais,”amesema.
Amesema Flattey ni kada mzoefu ndani ya CCM akianzia ngazi ya chipukizi na baadae kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM akiwakilisha wilaya ya Mbulu kabla ya kuwa mbunge kwa miaka kumi lakini pia alishakuwa mkiimbiza mwenge kitaifa hivyo kukimbilia upinzani ilikuwa ni kughafilika na msongo wa mawazo aloupata baada ya jina lake kutorudishwa.
Akizungumzia tathmini ya kampeni zinazoendelea, Wassira amesema wananchi wengi wanajitokeza kwenye kampeni za CCM kwa kuwa wanakiamini Chama pamoja na wagombea wake na zaidi ni utekelezaji mzuri wa ilani ya uchaguzi iliyopita.
Amesema CCM chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan mambo mengi yametekelezwa kwa asilimia kubwa ikiwemo katika sekta za afya, maji, elimu, miundo mbinu ya barabara ambapo imeunganisha mikoa yote, reli, nishati na kilimo.
Amesema mfano maeneo yaliyokuwa hayana maji Kwa miaka mingi hususani katika mikoa ya Arusha na Manyara hivi sasa wanapata maji na kuwarahisishia utendaji wa kazi wa Kila siku
“ Nikiwa Waziri wa maji nilienda na timu yangu pale orkesumet makao makuu ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, watu walikuwa wanajaribu kuchimba visima vidogo vidogo kutafuta maji lakini hakuna, Leo hii ilienda utashangaa, Serikali ya Samia imewapelekea maji ikiyatoa umbali mrefu huko ruvu, Sasa kwanini watu wasiichague CCM,”amesema.
Makamu Mwenyekiti Wassira kabla ya kufanya kikao hicho alipata fursa ya kumnadi mgombea wa nafasi ya ubunge Jimbo la Arumeru mashariki Dkt Johannes Lucumay katika mkutano uliofanyika eneo la Ngaramtoni ambapo wagombea wote walioshindwa kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM akiwemo aliyekuwa mbunge Noah Laizer, aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya na mfanyabishara maarufu Lukumay walisimamishwa kumuombea kura Dkt.Lucumay na kutangaza kuvunja makundi.

