Rais Samia amwaga vitabu Jiji la Arusha.

Baadhi ya walimu wakuu wa shule mbalimbali za Jiji la Arusha wakipokea vitabu

 

Na Mwandishi  Wetu,

Arusha. 

Halmashauri  ya Jiji la Arusha imepokea zaidi ya vitabu laki moja vya kiada na ziada kwa shule zote za  msingi zenye mchepuo wa kiingereza na Kiswahili kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba. 

Akizungumza katika ugawaji wa vitabu hivyo kwa walimu wakuu wa shule za jijini hapo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. John Pima amesema haijwahi kutokea  kwa jiji jilo kupokea idadi kubwa ya vitabu kama ilivyo sasa.

“Hii ni jitihada za Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuhakikisha sekta ya elimu inakuwa nchini, hivyo nawaomba wana Arusha kutambua jitihada hizi na kumuunga mkono, na sisi kama Jiji hatutamuangusha, tunaahidi kufanya kazi kwa bidii na kwa ari zaidi” Alisema Dkt Pima.

Dkt Pima amesema wamepokea jumla ya vitabu 107,644 ambapo wamevigawa kwa shule zote za msingi zilizopo katika jiji hilo kwa maana ya shule zenye mchepuo wa kiingereza pamoja na zenye mchepuo wa Kiswahili kwa masomo mbalimbali.

Ameongeza kuwa pia vipo vitabu vya miongozo ya walimu, vitabu vya elimu maalum pamoja na vitabu ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA) na kwamba tayari ameshatoa maelekezo kwa walimu wakuu wa shule hizo kuvitunza ili viendelee kutumika kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi jiji la Arusha Mwl. Reginald Peter Richard amemuhakikishia Mhe. Rais kufanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba na kushika nafasi ya kwanza kitaifa kutoka nafasi ya pili walioshika katika matokeo hayo mwaka jana.

“Hili ni deni kwetu, kwani Mhe. Rais ametuwekea mazingira mazuri ya kuhakikisha sekta ya elimu inakua, niseme tu kuwa hata hii nafasi ya pili tulioshika mwaka jana siyo sawa, sisi tulipaswa kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwani hatuoni sababu ya kushindwa kutokana na kuwepo kwa miundombinu bora ya elimu” Alisema Mwl Richard

Amesema moja ya mikakati ya kuhakikisha kuwa jiji hilo linashika nafasi hiyo ni pamoja na kubuni mbinu mbalimbali za ufundishaji zitakazosaidia stadi za KKK, kudhibiti tatizo la utoro na tayari wameshaweka mkakati na wazazi ili wanafunzi waweze kupata chakula cha mchana.

Aidha amesema ameshatoa maelekezo kwa walimu hao kuweka utaratibu wa kuwaazimisha wanafunzi vitabu hivyo ili waweze kujisomea majumbani siku za mwishoni mwa mwiki badala ya kuwaacha kutumia muda huo kucheza.

Mstahiki Meya wa Jiji hilo Maximilian Iraghe amesema licha ya vitabu hivyo kuwasaidia wananfunzi katika masomo yao lakini pia vitatoa motisha kwa walimu katika ufundishaji kwani hapo awali walimu hao walikabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitabu vya miongozo na ufundishaji.

Baadhi ya walimu waliozungumza wakati wa upokeaji wa vitabu hivyo. Mwl. Zebedayo Mollel Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Themi pamoja na Mwl. Zukra Karunde Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Daraja Mbili walisema serikali itegemee mabadiliko makubwa kwenye suala la kitaaluma.

Walisema awali kitabu kimoja kilikuwa kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya tano lakini kwa idadi ya vitabu walivyopokea kitabu kimoja kitatumiwa na mwanafunzi mmoja au wawili tu.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post