WATU 1800 KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI KIJIJI CHA MPONDA SUMBAWANGA

 Na Mwandishi Wetu, Rukwa

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Sumbawanga umefanikiwa kukamilisha mradi wa maji utakaonufaisha wananchi wapatao 1820 wa kijiji cha Mponda Manispaa ya Sumbawanga.

Akizungumza kwenye ukaguzi wa mradi huo jana (18.01.2022) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliwataka wananchi hao kuutunza mradi huo kwa kupanda miti kwenye chanzo cha maji ili kulinda na kuhifadhi mazingira hatua itakayofanya maji yawe endelevu.

Mkirikiti aliwataka pia wahandisi wa RUWASA kukamilisha miundombinu ya mradi huo ikiwemo ujenzi wa vituo vyote 12 vya kuchotea maji na kuweka koki pamoja na kufikisha maji kwenye eneo la ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho cha Mponda.

“Ruwasa nataka mtumie kipindi hiki kifupi kuhakikisha maji yanafika kwa walengwa kijijini pamoja na eneo panapojengwa zahanati ya kijiji cha Mponda ili yarahisishe kazi hatua itakayosaidia spidi ya mradi huo” alisisitiza Mkirikiti.

Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza pia suala la RUWASA kushirikiana na uongozi wa msitu wa Mbizi kupanda miti rafiki kwa mazingira katika eneo la chanzo cha maji hayo ili kuhifadhi mazingira katika kipindi hiki cha mvua.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Meneja wa RUWASA Sumbawanga Mhandisi Bahati Haule alisema mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Machi 2021 kwa gharama ya shilingi 240,683,948 kwa mfumo wa Force Account na unatarajia kukamilika mwisho mwa mwezi Januari 2022.

Mhandisi Haule alieleza kazi zilizofanyika kuwa ni ujenzi wa chanzo (intake), ujenzi wa nyumba ya mitambo, kufunga mfumo wa umeme wa jua, kufunga pampu ya kusukuma maji na ujenzi wa tanki lenye uwezo wa lita 150,000.

“Hadi sasa tayari asilimia 98 ya mradi umekamilika na Ruwasa tumefanikiwa kusambaza maji kwa wananchi kupitia vituo vya kuchotea maji 8 kati ya 12 pamoja na uchimbaji na ulazaji bomba kwenye mitaro umbali wa mita 6,116 ambapo jumla ya watu 1820 wa kijiji cha Mponda watanufaika kwa kupata maji safi na salama” alisema Mhandisi Haule.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alikagua miundombinu ya barabara zinazojengwa  kwa lami na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ambapo alikagua mradi wa barabara ya Baruti na Nyerere yenye urefu wa mita 350 inayojengwa na mkandarasi M/s Sumry Enterprises Ltd kwa Gharama ya shilingi 237,370,330 iliyofikia asilimia 95 ya ujenzi.

Akizungumza kwenye ziara hiyo Meneja wa TARURA Wilaya ya Sumbawanga Mhandisi Samson Kalesi alitaja barabara nyingine inayojengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni barabara ya Petrol Station hadi High Court yenye urefu wa kilometa moja chini ya mkandarasi M/s Sumry Enterprises Ltd kwa gharama ya shilingi 499,822,820 iliyofikia asilimia 95 ambapo itakamilika Mei mwaka huu.

Mkirikiti aliwapongeza TARURA kwa kazi nzuri ya kusimamia matumizi ya fedha za serikali ambapo ameridhishwa na namna mkandarasi alivyojenga barabara hizo na kutaka azikamilishe kwa viwango vilivyokusudiwa ikiwemo mitaro ya kupitisha maji na alama za barabarani.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post