CORONA YAKWAMISHA MAPAMBANO DHIDI YA MALARIA: WHO

 Na Mwandishi Wetu, Arusha

Wakati mlipuko wa ugonjwa wa homa ya Mapafu ( Covid - 19), ukielezwa kumalizwa nchini kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli, shirika la Afya Duniani, limesema ugonjwa huo ambao umeendelea kuua maelfu wa watu duniani unakwamisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.

Shirika la WHO limeonya kuwa kutokana na kulishughulikia zaidi janga la virusi vya corona huenda kukawa na hadi vifo 100,000 zaidi vitokanavyo na ugonjwa wa malaria kwa mwaka huu.

 

Katika ripoti yake ya mwaka kuhusu ugonjwa wa malaria duniani iliyotolewa Novemba 30, 2020, WHO imesema maendeleo ya kupambana na ugonjwa huo yamekwama katika miaka ya hivi karibuni hasa katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kuna visa vingi pamoja na vifo.

Mbu aina ya anopheles wa kike. mbu huyu ndio anayeambukiza ugonjwa wa Malaria

 

WHO imesema mwaka 2019 kulikuwa na takriban maambukizi milioni 229 ya malaria duniani, takwimu ambazo zilikuwa sawa na za miaka minne iliyopita na kwamba vifo vya malaria vinaweza kuzidi vile vitokanavyo na janga la COVID-19, huku wengi wao wakiwa watoto.

 

Kwa mujibu wa shirika hilo, watu 409,000 duniani walikufa kwa ugonjwa wa malaria mwaka 2019, wengi wao wakiwa kutoka maeneo masikini ya Afrika, ikilinganishwa na watu 411,000 kwa mwaka 2018.

 

Hata hivyo, ripoti hiyo imesema kuwa kampeni nyingi za kupambana na malaria ziliendelea wakati huu ambapo janga la virusi vya corona limeendelea kuua maelfu wa watu duniani, lakini kuna wasiwasi kwamba juhudi za kukabiliana na malaria zinaingiliana na mzozo wa COVID-19 ambao unakwamisha juhudi hizo na kurudisha nyuma zaidi mapambano.

 

Mkurugenzi wa WHO anayehusika na mpango wa malaria, Pedro Alsonso, amesema kutokana na mzozo wa corona, nchi nyingi zimefunga mipaka yake na viwanda hatua ambayo pia inazuia au inakwamisha kupelekwa kwa vyandarua vya kujikinga na mbu pamoja na dawa za malaria.

 

Aidha, serikali zimezielekeza rasilimali zake katika kupambana na janga la COVID-19, ambazo pia zilikuwa ni gharama za kupambana na malaria.

Mkurugenzi wa WHO barani Afrika, Matshidiso Moeti amesema virusi vya corona vinatishia kukwamisha juhudi za kupambana na malaria. Moeti amesema licha ya COVID-19 kuuathiri uchumi wa Afrika, washirika wa kimataifa wanahitaji kuongeza juhudi kuhakikisha kwamba rasilimali zinaongezwa katika miradi ya malaria ambayo inaleta mabadiliko.

 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Gebreyesus amesema ni muda kwa viongozi wa Afrika na dunia kwa ujumla kuamka tena na kupambana na malaria. WHO imesema upungufu wa fedha za kupambana na malaria unaleta kitisho kikubwa, huku ikiwa na dola bilioni 3 kati ya dola bilioni 5.6 zilizochangishwa 2019.

 

Zaidi ya asilimia 90 ya ugonjwa huo uko barani Afrika, ambapo takwimu zinaonyesha watu 384,000 walikufa mwaka uliopita 2019 huku nchi kama Nigeria ikitajwa kuwa na asilimia 27 ya vifo hivyo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo asilimia 12, Uganda asilimia tano na Msumbiji asilimia nne.

 

Kwa mujibu wa aliyekuwa waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto Ummy Mwalimu alipokuwa akiwasilisha bajeti ya Wizara Juni mwaka huu, 2020, Maambukizi ya Malaria yamepungua kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 7.3 Machi 2020. Aidha, vifo vitokanavyo na malaria vimepungua kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi kufikia vifo 2,079 Machi 2020.

 

Aidha ripoti ya WHO imesema nchi 21 zimefanikiwa kuutokomeza ugonjwa wa malaria katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Nje ya Afrika, India imeendelea kupata faida kubwa katika miaka miwili iliyopita, huku ikipunguza asilimia 18 ya maambukizi na asilimia 20 ya vifo.

 

Peter Sands, Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa dunia wa kupambana na UKIMWI, kifua kikuu na malaria amesema ripoti ya WHO imetolewa kwa wakati unaofaa.

 

Hata hivyo wakati WHO ikitoa takwimu na taarifa yake, nchini ugonjwa wa Malaria umeendelea kuthibiwa kwa hatua mbalimbali ikiwemo kunyunyiziwa kwa dawa kwenye mazalia ya mbu katika maeneo ambayo yameonekana kuwa hatarishi.

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post