Na Seif Mangwangi, APC Media, Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema malezi bora ya watoto ni msingi wa kujenga familia imara, jamii yenye maadili na hatimaye Taifa lenye uwezo wa kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo Septemba 23, 2026, mjini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Nusu Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM), unaofanyika kwa siku tatu na kuwakutanisha washiriki 340 kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali.
Amesema mkutano huo ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa programu hiyo, kubaini changamoto zilizopo na kukubaliana hatua za kuzitatua, huku akisisitiza kuwa kila mkoa unapaswa kuondoka na vipaumbele vya wazi, mpango kazi unaotekelezeka na namna ya kupima mabadiliko yanayopatikana katika maisha ya watoto na familia zao.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kaulimbiu ya mkutano huo ya “Malezi Bora ya Mtoto Kufikia Dira ya Taifa 2050” inasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika maisha ya mtoto wa leo, akieleza kuwa mtoto anayepata lishe bora, huduma za afya, ulinzi, nafasi ya kucheza na kujifunza pamoja na malezi yenye upendo huwekewa msingi wa kuwa mtu mwenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan Nguzo ya Pili inayohusu maisha bora na ustawi wa watu, inaweka wajibu wa kuwekeza katika maendeleo ya binadamu kuanzia hatua za mwanzo kabisa za maisha, huku akisisitiza kuwa malezi na makuzi ya mtoto yanahitaji ushirikiano wa familia, jamii, vituo vya huduma na Serikali.
Dkt. Gwajima amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ilikuwa na watu 61,741,120, huku Tanzania Bara ikiwa na watu 59,851,347, na kwamba watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi minane wanakadiriwa kuwa takriban milioni 16, hali inayodhihirisha ukubwa wa wajibu wa kuhakikisha kundi hilo linapata huduma bora.
Amesema huduma hizo zinapaswa kujumuisha afya, lishe, malezi, ulinzi na ujifunzaji wa awali, huku akisisitiza umuhimu wa kuunganisha huduma hizo ili kuhakikisha mtoto, hasa mwenye ulemavu au aliye katika mazingira hatarishi, hapotezi fursa ya kupata huduma kwa sababu ya kutokuwepo kwa uratibu wa mifumo.
Waziri huyo amesema Serikali inaandaa "Jamii Ajenda 2050" ambayo inalenga kutoa mwelekeo wa pamoja wa kujenga ustawi wa watu na uimara wa jamii katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akieleza kuwa katika eneo la mtoto, ajenda hiyo inahitaji kuimarisha familia, kulinda utu na usalama wa mtoto, kujenga maadili na kuhakikisha huduma zinazomhusu mtoto zinafanya kazi kwa pamoja.
Amesema familia inapaswa kuwa kitovu cha malezi, huku wazazi na walezi wakibeba nafasi ya kwanza katika kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira yenye upendo, ulinzi na mwongozo, na kwamba Serikali, taasisi za dini, shule, vituo vya afya, vyombo vya habari na wadau wengine wanapaswa kutoa msaada unaoiwezesha familia kutimiza wajibu huo.
Dkt. Gwajima ametaja umuhimu wa malezi katika kujenga maadili ya watoto, akisema watoto wanahitaji kufundishwa kusema ukweli, kuheshimu wengine, kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika, kusaidiana na kuipenda nchi yao, huku akibainisha kuwa maadili hayo hujengwa kupitia maneno pamoja na mifano wanayoiona kutoka kwa wazazi, walezi, viongozi na jamii inayowazunguka.
Amesema Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto imekuwa ikitekelezwa tangu Desemba 2021 na kwamba tathmini inayofanyika inapaswa kuangalia iwapo huduma zilizopangwa zinawafikia watoto, ubora wa huduma hizo na namna zinavyowafikia watoto ambao wako katika mazingira ya hatari ya kuachwa nyuma.
Katika tathmini hiyo, Waziri amewataka washiriki kuangalia pia upatikanaji wa huduma kwa watoto wenye ulemavu na mahitaji maalum, maarifa na msaada wanaopata wazazi na walezi, usalama na ubora wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana pamoja na namna takwimu zinazokusanywa zinavyotumika katika kufanya maamuzi na kuboresha huduma.
Dkt. Gwajima ametoa maelekezo kwa mikoa na halmashauri kuhakikisha huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto zinaingizwa katika mipango na bajeti zao, huku akitaka masuala ya watoto yawe ajenda ya kudumu katika vikao vya mikoa, wilaya na halmashauri ili kufuatilia utekelezaji, changamoto na uwajibikaji.
Aidha, ameitaka Serikali za Mitaa kusimamia ubora wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, kuimarisha mafunzo kwa wazazi, walezi na watoa huduma kuhusu malezi chanya na lishe, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa ukuaji wa mtoto na mifumo ya ulinzi ili mtoto anayehitaji msaada aweze kupata huduma kwa wakati.
Waziri huyo pia amewataka wadau wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utafiti, mafunzo, ubunifu na utoaji wa huduma, huku akisisitiza umuhimu wa Tanzania kujenga uwezo wake, kuweka rasilimali na kuimarisha mifumo endelevu ya kuwahudumia watoto hata pale miradi ya wadau inapomalizika.
Amesema matarajio yake ni mkutano huo wa siku tatu kuhitimishwa kwa mapendekezo yanayotekelezeka kwa awamu inayofuata ya PJT-MMMAM, huku kila mkoa ukiwa na mpango kazi unaobainisha vipaumbele, wahusika, muda wa utekelezaji na namna ya kuthibitisha mabadiliko katika maisha ya watoto, akihitimisha kwa kauli kwamba “Tukimlea mtoto vizuri leo, tunaiimarisha familia yake; tukiziimarisha familia zetu, tunaijenga jamii yenye maadili na mshikamano.”
