SERIKALI YAAGIZA HATUA KALI ZICHUKULIWE KWA WAKAGUZI WA UGAVI NA MANUNUZI AMBAO HAWAJASAJILIWA NA BODI YA PSPTB

Na Seif Mangwangi, APC Media - Arusha

SERIKALI imeiagiza bodi ya manunuzi na ugavi nchini, (PSPTB), kuwachukulia hatua za kisheria maafisa wote wanaofanyakazi ya ukaguzi bila kusajiliwa na bodi hiyo ya manunuzi.

Aidha bodi ya PSPTB imeagizwa kukaa pamoja na PPRA kuhakikisha wataalam wote wanaofanya shughuli za  ununuzi na ugavi waweze kuratibiwa na mfumo kama ilivyokusudiwa.

" Vile vile ninawaagiza waajiri wote hapa nchini wahakikishe wanawatumia wataalam wanaotekeleza shughuli za ugavi na ununuzi katika taasisi zao wawe wamesajiliwa na bodi ya PSPTB kama Sheria no23 ya PSPTB ya mwaka 2007 inavyoelekeza, hii itasaidia kuleta weledi na wajibikaji katika utendaji wa kifanisi katika sekta zote hapa nchini,".

Agizo hilo limetolewa leo Disemba 19, 2025 na Naibu Waziri wa Fedha Mhandisi Msham Ally Munde akimwakilisha Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Omar Chande katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano la 16 la maafisa manunuzi na ugavi linaloendelea katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano AICC.

Naibu Waziri Munde amesema kumekuwepo na maafisa manunuzi na ugavi ambao hawajasajiliwa na bodi ya PSPTB kama Sheria inavyowataka jambo ambalo halikubaliki.


“ Moja ya kazi ya bodi ya PSPTB ni kusimamia na kudhibiti masuala ya maadili na uadilifu na ndio sababu maafisa wote wanatakiwa kusajiliwa na bodi lakini kumekuwepo na maafisa wanaofanyakazi bila kusajiliwa, naagiza fanyeni ukaguzi mkiwakamata wachukuliwe hatua za kisheria,” amesema.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya PSPTB Jacob Kibona amesema bodi yake imeendelea kusimamia kufanyika kwa ukaguzi wa ukidhi wa sheria ya PSPTB, kuhakikisha shughuli za ununuzi na ugavi zinafanywa na wataalam wenye sifa stahili. 

Amesema katika kaguzi zilizofanywa bodi hiyo imebaini kuwepo kwa upungufu mkubwa wa wataalam wenye sifa, hususani katika Halmashauri za Miji, Wilaya na Manispaa nchini. 

“Sanjari na hilo upungufu wa watumishi wenye sifa umesababisha baadhi ya Halmashauri kutumia watumishi ambao ni nje ya taaluma ya ununuzi na ugavi kinyume na kifungu cha 11 cha sheria ya PSPTB,” amesema.

Amesema ukiukwaji huo wa Sheria ni hatari kitaaluma na utendaji wenye tija katika eneo la ununuzi na ugavi na matokeo yake ni kusababisha upotevu wa fedha za umma na hivyo kuzalisha hoja nyingi za ukaguzi kila mwaka. 

“Hata hivyo, PSPTB kwa kushirikiana na mamlaka husika imekuwa ikifanya kazi na Wizara yako kutafuta suluhu ya changamoto hii. Ni matumaini yetu kuwa serikali italitafutia ufumbuzi suala hili kwa kuendelea kuajili wataalam wa ununuzi na ugavi hususan katika ngazi mbalimbali chini za Serikali za Mitaa,” amesema.

Amesema Ukaguzi wa wataalam unaoendelea kufanywa na Bodi ya PSPTB umebaini baadhi ya taasisi binafsi kutozingatia ukidhi wa sheria ya PSPTB kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 11 na 40 cha Sheria Na 23 ya Mwaka 2007. 


 

Aidha amesema bodi ya PSPTB imefanikwa kuwajengea uwezo wataalam wake na wadau wa mnyororo wa ugavi katika taasisi za umma na binafsi ili kuendana na mabadiliko ya kitaaluma na kiutendaji. 

Amesema kupitia mafunzo hayo katika mwaka wa fedha 2024/2025 PSPTB imefanikiwa kuwajengea uwezo Wataalam 3,164 kutoka katika sekta ya umma na binafsi.


Aidha Kibona amesema PSPTB imeanzisha mafunzo ya wakaguzi katika ununuzi na ugavi ikiwa sehemu ya utekelezaji wa mtaala wa kitaaluma na vigezo vya usajili kitaaluma. 

“Bodi imefanya jitihada hizi ili kuinua umahiri wa wataalam wa ununuzi na ugavi katika ujuzi wa ukaguzi wa mnyororo wa ugavi na mbinu za ukaguzi. Hii itasaidia watalaam hawa kuweza kuleta tija kwenye ukuguzi wa mnyororo huu wa ugavi na kukuza weledi wao kama wakaguliwa wanachotakiwa kuwajibika katika kaguzi husika,” Amesema.

Amesemani matarajio ya bodi kuwa wadau wa ukaguzi katika mnyororo wa ugavi watawatumia wataalam waliosajiliwa na kuidhinishwa na Bodi katika ukaguzi wa mnyororo wa ugavi katika kaguzi za ndani na kaguzi za nje ili kuendelea kudhibiti fedha za umma katika ununuzi wa umma na usimamizi.


Kibona amesema pamoja na jitihada zinazoendelea kufanywa na bodi hiyo bado wataalam wa ununuzi na ugavi wamekuwa wakipata Maslahi madogo ukilinganisha na taaluma zingine.

Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri wa Mhandishi Munde amesema wizara imeshasikia changamoto hizo,  zinaendelea kufanyiwa kazi na kwamba kabla ya Bajeti ijayo zitakuwa zimeshapatiwa ufumbuzi.

Katika kongamano Hilo wadau mbalimbali wanashiriki ikiwemo wataalam kutoka shirika la nyumba la Taifa NHC ambapo pia Naibu Waziri alipata fursa ya kutembelea mabanda ya maonyesho.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post