Serikali yatakiwa kuwashirikisha wataalam wa kilimo kufufua zao la Shayiri

 


 

Na Claud Gwandu, Arusha

  

SERIKALI imetakiwa kuwashirikisha kikamilifu  wataalam wa kilimo hasa watafiti katika kuendeleza kilimo cha Shayiri ambacho ni zao muhimu la biashara.

 

Shayiri ni zao linalofanana na ngano ambalo hutumika kama malighafi ya kuzalisha kinywaji cha bia ambacho hutumiwa na watanzania wengi.

 

Mratibu wa zao la Shayiri nchini, Salome Munisi anasema kuwa kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa Shayiri nchini kinatisha na kwamba hatua za makusudi lazima zichukuliwe kuliokoa zao hilo.

 

 

Salome ambaye pia ni mtafiti katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Selian kilichopo jijini Arusha, aliwaambia wanahabari walioshiriki mafunzo ya sayansi na utafiti yaliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) iliyofanyika jijini hapa hivi karibuni kuwa  mahitaji ya zao hilo nchini ni makubwa lakini uzalishaji ni mdogo.

 

“ Inasikitisha kuona zao ambalo lilikuwa tegemeo la wakulima katika baadhi ya mikoa nchini sasa limesahaulika na Shayiri karibu yote inabidi iagizwe nje jambo ambalo halina tija kwa uchumi wa nchi na wakulima,” anasisitiza Mratibu huyo .

 

Akitoa takwimu, mtafiti huyo anaeleza kuwa asilimia 80 ya mahitaji ya shayiri nchini inaagizwa kutoka Kenya na Afrika Kusini anaeleza kuwa,hali hiyo haina tija wala manufaa kwa nchi na wakulima wa zao hilo.

 

Alitoa sababu ya kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo pamoja na ngano kuwa ni kukosekana kwa mipango endelevu ya kusaidia wakulima ikiwa ni pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakika.

 

Hata hivyo,Serikali imekuwa ikisisitiza kuwasaidia wakulima wa ngano na shayiri na kutengenezea mazingira mazuri wakulima wa shayiri na ngano ili wapate masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

 

Takwimu zinaonyesha kuwa uzalishaji wa shayiri nchini kwa mwaka 2020 ulikuwa tani 20 392   ambao ni ongezeko kidogo ulikinganisha na miaka ilittopita.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO),uzalishaji wa shayiri ni mdogo nchini pamoja na kwamba Tanzania ni miongoni mwa mataifa 86 duniani yenye mazingira bora ya kuzalisha zao hilo.

 

Zao hilo nchini linalimwa kwa wingi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambako wakulima huvuna wastani wa kilo 500 kwa eka ingawa wataalam wa kilimo wanasema kuwa uwezekano wa mavuno kufikia hadi kilo 1000 kwa eka,iwapo hatua madhubuti zitachukuliwa, upo.

1 Comments

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post