Mkuu wa Wilaya ya Mlele Alhaji Mwanga atajwa Uenezi CCM

 Na Mwandishi Wetu

Dodoma

Alhaj Majid Hemed Mwanga Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi ni miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi anayetajwa kuweza kurithi nafasi ya Katibu wa Uenezi na Itikadi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Jana, makada wa CCM wamesema Alhaj Majid Mwanga ni miongoni mwa vijana wasomi na wenye uzoefu wa uongozi ndani ya Chama hicho.

Majid Mwanga kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele alishawahi kuziongoza Wilaya za Lushoto Mkoani Tanga , Bagamoyo Mkoani Pwani na Kilosa Mkoani Morogoro kwa nyakati tofauti chini ya uongozi wa Marais Dkt Jakaya Kikwete na Hayati Dkt John Pombe Magufuli na Sasa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Jeremia Mollel mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Arusha amesema Majid ni kiongozi asiyekuwa na makundi ndani ya CCM tofauti na wajumbe wengine wanaotajwa hivyo anafaa kupewa nafasi ya Uenezi au Katibu Mkuu wa UVCCM.

"Mimi namjua vizuri sana Majid Mwanga, amekua ndani ya CCM kwa miaka mingi na ni kiongozi asiyekuwa na makundi, sisi Wana CCM tunataka vijana kama hawa ambao hawawezi kutugawa, namuomba Mwenyekiti wangu wa Chama Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika teuzi zake akumbuke jina la huyu kijana,"amesema.

Zaynab Hashim mjumbe na Mwanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Wilaya ya Lushoto anasema Majid Mwanga ni kijana mtaratibu na mchapakazi ambaye anastahili kupewa wadhifa mkubwa ndani ya CCM

"Majid ni miongoni mwa vijana wachapakazi sana hapa nchini na wasiokuwa na makundi, nimemfahamu tangu akiwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto,  baadae Bagamoyo na Kilosa na hivi Sasa Mlele, wananchi wanampenda na sisi tunampenda kwa kuwa anasikiliza kero za wananchi na anazitatua,"amesema Zaynab.

Kada wa CCM ambaye pia ni mtumishi Halmashauri ya Meru Wilayani Arumeru, Lily Msemo anasema Alhaj Majid anafaa kuwa kiongozi wa juu zaidi ya Ukuu wa Wilaya kutokana na uzoefu aliokuwa nao tangu alipoanza safari yake ya maisha kwenye siasa.

" Mimi namjua Majid tangu akiwa hapa Tengeru kama mwanachuo lakini alikuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya wanafunzi, amekuwa na misimamo yake imara hasa katika kutetea maslahi ya watu, yuko tayari kugombana na wewe ili watu wapate haki, ndani ya Siasa hilo ndio tunalitaka, na hakika amekuwa mtetezi mzuri, kule Bagamoyo na Kilosa alipambana na wafugaji na wakulima akaweza kupunguza vurugu na Sasa yuko Mlele,"amesema Lily.

Kada wa CCM Wilaya ya Kilosa aliyejitambulisha kwa jina la Said Salum na yeye kwa upande wake amemtaja Alhaj Majid Mwanga kama mmoja wa makada wa CCM wenye uwezo wa kushika nafasi zilizokuwa wazi ndani ya CCM kufuatia uteuzi uliofanywa hivi karibuni na Rais SAMIA Suluhu Hassan.

"Nimekaa na Majid hapa Kilosa kama Mkuu wangu wa Wilaya, amekuwa akifanyakazi nzuri sana na wananchi walikuwa wanampenda, alifika vijiji vingi ambavyo havikuwahi kufikiwa lakini pia aliweza kutatua kero nyingi hasa ugomvi wa wakulima na wafugaji, kwa maoni yangu anaweza kushika nafasi zilizowazi kama akipewa nafasi na Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wangu wa Chama Dkt Samia Suluhu Hassan,"Amesema Salum.

Makada wengine wanaotajwa kuweza kushika nafasi ya Uenezi iliyokuwa chini ya Paul Makonda aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla, Alli Happi aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa na Lengai Ole Sabaya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai kabla ya kutenguliwa.

Majid Mwanga ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa , kupitia Wilaya ya Kilosa kabla ya kuteuliwa kuanza kushika nafasi za Ukuu wa Wilaya, alishakuwa mjumbe wa kamati ya Siasa ya Mkoa na mjumbe wa kamati ya maadili ya Mkoa chini ya Mwenyekiti wa UWT hivi Sasa na Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda ambaye wakati huo alikuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post