Na Claud Gwandu, Arusha
MCHANGANYIKO wa aina mpya ya mbegu za maharagwe umeelezwa kuwa tumaini jipya kwa watu wenye changamoto za uzazi, wakiwamo wanaume na wanawake wajawazito
Mbegu hizo mpya zilizogunduliwa hivi karibuni na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian(TARI-Selian) kilichopo Arusha zinaelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa kurutubisha na kuongeza uzazi kwa watu wenye changamoto hizo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mpango wa Maharage katika Kituo hicho, Nestory Shida, matokeo chanya ya mbegu za maharage hayo yameanza kuonekana katika mikoa kadhaa ambako sasa ni lulu.
Anasema mchanganyiko wa mbegu hizo uliogunduliwa na kituo hicho mwaka 2018 hicho, umeonyesha matokeo mazuri katika mikoa ya Dodoma, Singida, Iringa na Mbeya.
Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga nayo imechangamkia aina hiyo mpya ya mbegu za maharage
Mtafiti huyo alisema katika mafunzo ya waandishi yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH) yaliyofanyika jijini hapa hivi karibuni kwamba maharage hayo yana madini aina ya chuma na zinki ambayo yanachochea hamu ya tendo la ndoa na kuongeza mzunguko wa damu kwa wanawanake wajawazito
“Maharage hayo yanayoitwa Selian 14, 15 na Jesca yamekuwa kimbilio la wengi katika mikoa niliyotaja kutokana na matokeo yake mazuri katika masuala ya uzazi ambayo yamekuwa na changamoto nyingi na sasa ni kimbilio la wengi,” Shida aliwaambia waandishi waliokuwa katika mafunzo hayo walipotembelea kituo hicho na kuongeza:
“Mchanganyiko wa mbegu hizi umethibitisha kusaidia kutibu tatizo la wanaume kushindwa kushiriki kikamilifu tendo la ndoa au upungufu wa nguvu za kiume (ED) na kuboresha uwezo wa wanawake wajawazito katika kutunza na kulea mimba.”
Kwa mujibu wa mtafiti huyo, majaribio ya mbegu hizo yamethibitisha kuwa madini yaliyo ndani ya mbegu hizo yana uwezo wa kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume wenye upungufu lakini pia kusaidia mzunguko wa damu kwa wanawake wajawazito.
Upungufu wa nguvu za kiume (ED) ni tatizo linalowakabili wanaume wengi kutokana na sababu mbalimbali na linachangia kuvunjika kwa ndoa nyingi.
Madini ya zinki yanasaidia kuongezeka kwa homoni zinazosaidia kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la upungufu wa nguvu wakati madini ya chuma yanasaidia mzunguko mzuri wa hewa ya oksijeni mwilini.
Aidha, Mtafiti huyo anaongeza kuwa aina hiyo ya mbegu za maharagwe ni muhimu pia katika kusaidia tatizo la utapiamlo miongoni mwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano na kwa wanawake wanaonyonyesha.