"Mkurugenzi Mtendaji anasikitika kuwafahamisha kuwa, ratiba ya ziara ya leo ya kukabidhi miradi yetu kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imeahirishwa ghafla.

"Hii ni kutokana na ajali mbaya iliyoukumba msafara wa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wakati akiwa anakuja ambapo gari lilokuwa limebeba kikosi cha waandishi wa habari limegongana na Hiace uso kwa uso maeneo ya Busega.

"Taarifa zinasema kuwa watu watano wamepoteza maisha ambao inasemekana kuwa ni waandishi na maafisa habari ndani ya mkoa wetu na pia inasemekana kuwa mojawapo ya waliofariki ni pamoja na ofisa habari na mahusiano wetu, Bw.Stephen Msengi.

"Taarifa zaidi zitaendelea kutolewa na kuthibitishwa. Kufuatia hali hiyo, uongozi wa mkoa na wilaya umeamua kusitisha ratiba ya ziara hii hadi siki nyingine itakayopangwa.Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amen

Awali, Edwin Soko ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Mwanza amebainisha kutokea kwa ajali hiyo na yuko njiani kupelekea eneo la tukio kwa uthibitisho zaidi.


"Nimeongea na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ndugu Gabriel amethibitisha kutokea taarifa za watu watano waliokuwa kwenye gari hilo lililobeba waandishi kufariki.Majina ya wenzetu hao tutayatoa kadri tutakavyofuatilia.

"Kwa sasa Mkuu wa Mkoa nae anaelekea eneo la tukio nasisi pia tuko njiani kwenda eneo la tukio.Naomba tuwe watulivu kwa wakati huu, wakati team yetu na ya Mkuu wa Mkoa tunafuatilia tukio hilo,"amefafanua Soko.