MKUU WA MKOA WA ARUSHA KUWAPELEKA BODABODA RWANDA

Na Seif Mangwangi 

APC Media, Arusha. 

Mkuu wa mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla amesema atawapeleka madereva bodaboda na bajaji wa Mkoa wa Arusha, katika nchi za Rwanda na Uganda Ili wajifunze namna maafisa usafirishaji wa nchi hizo wanavyofanya kazi yao kwa ufanisi.


Akizungumza na maafisa usafirishaji hao leo Disemba 15, 2025 alipokuwa akisikiliza kero wanazokabiliana nazo, CPA Makalla amesema bodaboda wanatakiwa kuwa na utaratibu maalum Ili waweze kutekeleza majukumu yao.

Amesema bodaboda wa Arusha wamekuwa wakifanya kazi zao bila utaratibu maalum na kusababisha kero kwa wananchi hivyo wanatakiwa kutoka nje ya Arusha kujifunza.

“ Mimi nimetembea katika nchi za Rwanda na Uganda, ukifika kule bodaboda na bajaji Wana utaratibu mzuri sana wa kufanyakazi zao, wana vitambulisho, tofauti na sisi hapa kwetu, nitawapeleka kule mkajifunze” amesema.

Wakitoa malalamiko yao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, bodaboda wameushutumu uongozi wa bodaboda Mkoa wa Arusha kung’ang’ania kuongoza wakati hawatakiwi na kwamba uongozi wao umeonyesha kushindwa kuunganisha bodaboda hao.

Wamesema viongozi hao wameshindwa kuwaunganisha bodaboda kuanzisha ushirika wa bodaboda na kumuomba Mkuu wa Mkoa kuvunja uongozi huo na kuchukua fedha zilizopo kukopeshana. 

Mmoja wa waendesha bodaboda Kata ya Kimandolu Godlisten Evarest amemuomba mkuu wa mkoa kuwasaidia kupata viongozi wapya akiwemo mwenyekiti kufuatia mwenyekiti aliyekuwepo kupoteza maisha katika machafuko ya Oktoba 29.


"Nakuomba utusaidie kupata viongozi wapya maana hata waliobaki wanakula pesa zetu hawana msaada, tukihoji hawatoi majibu ya kueleweka, vile vile naomba Polisi waache kukamatakamata watu kwa kuangalia sura bali wazingatie makosa" amesema Godlisten. 

Vilevile Vedasto Msukuma afisa usafirishaji kata ya Ungalimited ameomba waendesha bodaboda na bajaji wote kuwa na vitambulisho vitakavyowatambulisha kwa wateja wao. 

Kero zingine walizowasilisha ni pamoja na kutokuwa na vituo maalum vya kupaki bodaboda na bajaji, kukosa mikopo, kusimamishwa hovyo na askari wa usalama barabarani na kukosa fedha kwaajili ya ununuzi wa sare zitakazowatambulisha endapo kutatokea changamoto yoyote.

Akijibu changamoto hizo, Mkuu wa Mkoa CPA Makalla amempatia Mkuu wa Wilaya ya Arusha siku saba kutatua changamoto ya uongozi kati ya bodaboda Mkoa wa Arusha na wilaya na baada ya kumaliza changamoto hiyo ampatie taarifa.

Kuhusu kero ya kukosa mikopo, CPA Makalla alimtaka Mkurugenzi wa Jiji kujibu hoja hiyo, ambapo Kwa niaba yake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Jiji la Arusha, Shabani Manyama alisema Jiji Hilo limekuwa likitoa mikopo Kwa wajasiriamali mbalimbali ikiwemo madereva bodaboda na bajaji.


Amesema kupitia asilimia kumi ya mapato ya Jiji, vikundi vya wanawake, vijana na walemavu wameshawezeshwa mamilioni ya fedha na kwamba Jiji linaendelea kutoa mikopo hiyo bila upendeleo wowote.

Akifunga kikao hicho cha uzinduzi wa kusikiliza kero za wananchi Jiji la Arusha, CPA Makalla amesema kero zilizowasilishwa zitapatiwa ufumbuzi mapema sana.

Amesema mfano kero ya ubovu wa Barabara katika Jiji la Arusha, Rais Samia Suluhu Hassan ameshalisikia na kuagiza lifanyiwe kazi.


“ Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye kampeni aliombwa Barabara na aliagiza akishaapishwa atataua kero hiyo, na mimi nilikuwa shahidi, naombeni mniachie nitatua,” ameahidi CPA Makalla.

Aidha amesisitiza suala la kauli nzuri kutoka kwa watumishi kuwapa nafasi wananchi kutoa maoni na kueleza changamoto zao zinazowakabili badala ya kuwakatisha tamaa na kupuuza changamoto zao. 

"Nawasihi itunzeni ahadi ya kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuendelea kusaidia wananchi wanaotumia vyombo vyenu vya usafiri, wanaovitumia hadi usiku wa manane wakiwemo mama ntilie, wagonjwa na wengineo", 


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post