DC MKUDE AWATAKA MADIWANI WAPYA KUTII KIAPO, KUACHA CHUKI,

 Na Seif Mangwangi, Arusha 

MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amewataka Madiwani wapya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuzingatia kiapo cha utii na maadili walioapa kwa kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha amewataka Madiwani hao kuondoa chuki dhidi yao na kulinda amani ya Tanzania kwa kile alichosema maendeleo yoyote duniani yanafanyika kwenye eneo tulivu na lenye amani.

DC Mkude ameyasema hayo Leo Disemba 4, 2025 alipokuwa akihutubia baraza jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha mara baada ya kumaliza kuapa.


Katika kikao hicho cha kwanza kilichohudhuriwa na mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha, jumla ya madiwani 25 wa Kata za Jiji la Arusha na madiwani 09 wa viti Maalum wamekula kiapo mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Boniface Semroki kama ishara ya kuanza majukumu yao. 

Madiwani hao pia kwa mara nyingine walimchagua aliyekuwa Meya wa Jiji hilo Maximilian Iranghe Kwa kura za ndio 33 kati ya kura 34 sanjari na Naibu Meya Julius Meideye aliyeibuka mshindi Kwa kura 31 kati ya kura 34.


Akitoa hutuba ya kufungua Baraza la kwanza la Madiwani, Meya Maxmillian Iranqhe aliwashukuru Madiwani wenzake Kwa kumuamini na kuwaahidi kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM Kwa nguvu zote.

Amesema katika baraza hilo jipya wataanzia pale walipoishia katika baraza lililopita ambapo suala la matengenezo ya barabara litapewa kipaumbele pamoja na kuboresha usafi na mazingira ya Jiji la Arusha. 

Aidha Meya Iranghe amewataka Madiwani kuhakikisha wanaweka kipaumbele ajenda ya vijana kwa kuweka mazingira rafiki ya kuwapatia fursa ya kujikwamua kiuchumi.

"Jiji letu linakadiriwa kuwa na idadi ya watu wapatao laki sita, kati yao vijana wakiwa ni asilimia 60 ya watu wote. Ndugu zangu katika baraza hili tuhakikishe tunaweka mazingira bora na rafiki kwa vijana ili wapate fursa ya kujikwamua na umaskini, "amesema Iranqhe.


Awali Katibu tawala wa wilaya ya Arusha Jacob Rombo, akizungumza katika Baraza hilo amewapongeza madiwani wote waliochaguliwa na kuwataka kuwa tayari kuwatumikia wakazi wa Jiji la Arusha.

Amesema kwa kipindi chote ambacho madiwani wamekuwa nje Mkurugenzi wa jiji la Arusha John Kayombo pamoja na wakuu wa idara wamehakikisha wanawatumikia wananchi ipasavyo.





This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post