WAZIRI MKUU ASEMA WANAOHAMASISHA MAANDAMANO WANANIA OVU

Seif Mangwangi, Arumeru

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wananchi kutoshiriki kwenye maandamano yanayopangwa kufanyika Disemba9, mwaka huu 2025 na kudai kushiriki kwenye maandamano hayo ni kuigawa nchi sanjari na kurudisha nyuma maendeleo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa wilaya ya Arumeru  leo Novemba 30, 2025 katika kituo cha  polisi Kikatiti ambapo pia alitembelea kituo hicho kilichokuwa kimechomwa moto wakati wa maandamano Oktoba29, 2025, Dkt. Nchemba amewataka watanzania kutowasikiliza wanaharakati.

Amesema wanaharakati ndio wanaohamasisha maandamano hayo na kusema watu hao wana lengo la kuharibu amani ya nchi iliyotengenezwa na kudumu kwa miaka mingi. 


"Kuna wanaharakati wanakaa nje ya nchi ndio wanaowashawishi watanzania mjitokeze kuandamana, msikubali maana madhara yakitokea wao na watoto wao wanakuwa salama," amesema.

Na kuongeza," Tazama mmechoma kituo cha polisi mlichojenga wenyewe je, mtapata wapi huduma? Amkeni ndugu zangu hapa ndo nyumbani hatuna mahala pa kwenda".

Katika ziara hiyo Dkt Mwigulu pia ametembelea mahakama ya mwanzo iliyoko katika Kata ya Maji ya chai na kituo cha  mafuta cha Total Energies Wilayani Arumeru vyote vikiwa ni miongoni mwa mali zilizochomwa moto katika vurugu Oktoba 29, 2025. 


"ikumbukwe nchi yetu ni ya kwanza Afrika kwa uzalishaji wa madini ya Uranium na ya tisa duniani, hivyo watu wabaya wanatamani kutuyumbisha ili wachukue madini yetu"amesisitiza.
Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba akisalimiana na viongozi wa Mkoa wa Arusha waliofika katika uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kumpokea.

Aidha Waziri Mkuu Dkt Nchemba amewataka watumishi kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua, kuwa na kauli nzuri kwa wateja na kutatua changamoto zinaziwakabili.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa wizara ya vijana kupita katika vijiwe vyote vya vijana na kukusanya maoni ili waangalie namna ya kuwasaidia kuinua uchumi wa vijana hao. 


Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Arusha CPA Makalla amesema hali ya utulivu na usalama katika mkoa wa Arusha imeimarishwa na watalii wanaendelea kuingia licha ya kwamba ni kipindi cha kupungua wageni "low season".

CPA Makalla ametoa onyo kali kwa wanaojiandaa kufanya maandamano kwamba wakifanya hivyo watakutana na mkono WA Sheria na kuagiza jeshi la polisi kutekeleza majukumu yao ya kulinda raia na mali zao ipasavyo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post