Na Seif Mangwangi, Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude amewataka wafanyabiashara ndani ya Jiji la Arusha kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, 2025 na kisha kurejea kwenye biashara zao ijapokuwa siku hiyo imetangazwa kuwa mapumziko kitaifa.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mkoa wa Arusha Leo 27 Oktoba 2025, DC Mkude amesema maandalizi yote ya kupiga kura yamekamilika na ulinzi umeimarishwa Kila kona kuhakikisha watu wanapiga kura Kwa amani na utulivu.
Amesema Kwa mujibu wa uandikishaji jimbo la Arusha mjini lina idadi ya wapiga kura zaidi ya laki nne (435, 199) wanapatikana katika mitaa 154 ambapo jumla ya vituo 1051 vimetengwa kwaajili ya watu kupigia kura.
“ Tuna jumla ya vituo vya kupigia kura 1051 ambavyo vitatumika na wapiga kura 435,199, tumeweka vituo vingi Ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuata kituo, Arusha tumewasogezea karibu Ili Kila mtu apige kura ambayo ni Haki yake kikatiba,” Amesema.
Amesema vituo hivyo pia vimesogezwa karibu Ili kuondoa usumbufu kwa makundi maalum kama wazee na walemavu ambao wamekuwa wakishindwa kufikia vituo kutokana na kuwa umbali mrefu.
DC Mkude amesema hana taarifa ya kuwepo Kwa maandamano siku ya uchaguzi na kwamba kama Kuna watu wanapanga kufanya hivyo hawatapata fursa kutokana na ulinzi mkubwa uliowekwa siku hiyo ya uchaguzi.
Amesema ameshakutana na makundi mbalimbali Jiji la Arusha ikiwemo viongozi wa dini, vijana kupitia makundi yao tofauti na wanasiasa na wamemuhakikishia kujitokeza kupiga kura Kwa amani na utulivu.
“ Nimeshakutana na makundi mbalimbali ndani ya Jiji la Arusha na kufanya nao mazungumzo ya amani, nimekutana na vijana wa bodaboda, wanasiasa na hata viongozi wa dini, tumekubaliana kulinda amani yetu,” Amesema.


