MCT KUENDESHA KLINIKI YA MSAADA WA KISHERIA KWA WAANDISHI WA HABARI ARUSHA

Na Mwandishi Wetu, APC TV

BARAZA la Habari Tanzania kesho Agoati 21, 2025 kupitia mawakili nguli nchini, litaendesha kliniki maalum ya msaada wa kisheria kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha lengo likiwa ni kuwaweka Sawa waandishi wa habari wa Mkoa huo katika kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu 2025.

Akizungumza leo Agosti 21, 2025 Jijini Arusha, alipokuwa akifungua mafunzo ya sheria kwa baadhi ya waandishi wa habari mkoani humo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Ernest Sungura amesema waandishi wa habari wanapaswa kujua sheria zinazowaongoza ili kujiweka Sawa na matukio mbalimbali yanayojitokeza ikiwemo uchaguzi mkuu.

Aidha amewataka wanahabari mkoani Arusha kuona umuhimu mkubwa wa kuwatumia wanasheria katika kazi zao kwa ajili ya usalama wa kazi zao  hasa katika kuelekea uchaguzi mkuu 2025 .

Sungura  amesema kupitia kliniki hiyo ambayo itafanyika katika ofisi za chama cha  waandishi wa habari Mkoa wa Chama (APC), mwandishi mmoja mmoja atapata fursa ya kuzungumza na mwanasheria kwa faragha kuhusu masuala ya kisheria yanayomtatiza. 

Sungura ameongeza kuwa, hatua hiyo inatokana na matukio ya historia yanayoonesha kwamba wakati wa uchaguzi mara nyingi waandishi wa habari hujikuta katika mazingira hatarishi ikiwemo kukamatwa, vitisho, na kufunguliwa mashtaka yanayohusiana na  utekelezaji wa majukumu yao kitaaluma. 

“Kwa mfano, ingawa Ripoti ya Ukiukwaji wa Uhuru wa Vyombo vya Habari ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) ya 2022, ilionesha kupungua kwa ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari kutoka matukio 119 mwaka 2018/19 hadi 18 mwaka 2022, bado  ukiukwaji upo, ambapo jumla ya matukio 27 yaliripotiwa mwaka 2024 na matukio  mengine 17 yameripotiwa kati ya Januari na Agosti 2025. 

Matukio haya ni pamoja na kukamatwa, vitisho, utekaji nyara, maonyo, kusimamishwa, na kuingiliwa kwa uhuru wa uhariri, ” amesema.

“Huduma hii ya kisheria kwa waandishi wa habari inatolewa kwa ufadhili wa wenzetu shirika la International Media Support (IMS).”

Pia, amesema, kuna umuhimu kwa wanahabari kuhakikisha wanakuwa na wanasheria ambao wataweza kuwashirikisha changamoto zao zinazowakabili na kuweza kupata ushauri wa kuepukana na madhara yanayoweza kuwatokea, hususani kipindi cha uchaguzi .

“Kutokana na changamoto hizo, MCT imekuja kutoa elimu kwa wanahabari kuhusu umuhimu wa wanahabari kuwashirikisha wanasheria kwenye kazi zao hasa katika kuelekea uchaguzi ujao,” amesema Sungura.
 

“Mwandishi wa habari unapaswa kuwa makini na unapoandika habari yoyote lazima uwe na utulivu wa akili katika utendaji wako,” amesema Sungura na kuongeza:

“MCT inaamini kwamba jitihada hizi zitachangia waandishi wa habari kufanya kazi kwa kujiamini, kuongeza uwezo zaidi wa kuripoti bila hofu, kwa weledi, huku wakijua kwamba kuna jukwaa la wanasheria wa haki za binadamu watakaowasaidia kisheria wanapokuwa kazini,” amehitimisha Sungura.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Arusha,Claud Gwandu amesema kuwa, matokeo ya mafunzo haya yanaonekana kwani ni muhimu sana kwao hasa katika kipindi hiki tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Gwandu amesema kuwa, ni muhimu sana kwa waandishi wa habari kufahamu watu muhimu wa kuwasaidia katika maswala  ya kisheria na changamoto mbalimbali.

“Sisi ambao tumepata fursa ya kunufaika na mafunzo haya tunaahidi kuwa mabalozi wazuri sana na tutaitumia elimu hii ipasavyo na kuangalia nafasi ya kusaidia wengine .”amesema .

“Tunashukuru sana MCT kwa mafunzo haya kwani yatakuwa historia kwa waandishi wa habari nchini na tunawaahidi kuyafanyia kazi mafunzo haya kwa weledi mkubwa.”amesema.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post