DIWANI: ELIMU KWA VIJANA KATA YA UNGA LIMITED IMEMALIZA MAKUNDI YA WEZI NA WAKABAJI

Egidia Vedasto

Arusha

Kata ya Ungalimited ambayo hapo awali ilikuwa tishio kwa wageni na wenyeji kutokana na kuwa na matukio ya kihalifu, kwa sasa ni salama kutokana na elimu ya polisi jamii, ulinzi shirikishi na ulinzi jamii. 

Diwani wa Kata hiyo Mahmoud Omary amewatoa hofu wakazi wa Mkoa wa Arusha kuwa Kata yake kwa sasa ni salama, hakuna matukio ya uhalifu. 

Akizungumza na Mwandishi wa APC Blog ofisini kwake, Diwani Mahmoud amesema kwa sasa  hali ya usalama ni imara ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo watu wengi walizoea kuwa eneo la wezi na wakabaji. 

"Kupitia ushiriki wangu wa polisi jamii, ulinzi shirikishi hadi nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mtaa na leo kuwa Diwani, ilitosha kujua namna ya kukabiliana na changamoto hizo ambapo kwa sasa inabaki historia"

"Elimu hiyo ilisaidia kutambua vijana waliokuwa tayari kufanya kazi, ila kutokana na ukosefu wa mitaji na msaada walijikuta katika makundi mabaya, ambapo kwa sasa wengi tumewajengea uwezo wako sokoni wanafanya biashara na wengine wamejikita katika ufundi" Amefafanua Mahmoud

Kwa upande wa maendeleo amesema Kata hiyo imefanikiwa kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Shule ya Sekondari Ungalimited pamoja na ujenzi wa vyumba vya kisasa katika shule ya msingi Ungalimited.

"Pia tumejenga vivuko katika mitaa mbalimbali na kuongeza samani mashuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata viti na meza ili kusoma katika mazingira rafiki" amesema Diwani huyo na kuongeza 

"Tunaishukuru Serikali Kuu, Halmashauri ya Wilaya, na Wadau mbalimbali wa maendeleo kwa mchango wao mkubwa ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kusukuma maendeleo haya mbele" , 

"Kipekee naushukuru mchango wa pesa za Uviko, Mfuko wa Mama na Mbunge kwa michango yao iliyofanya maendeleo yetu yaonekane" ameeleza Mahmoud.

Amewataka wananchi wa Kata hiyo kuendelea na moyo wa ushirikiano kama ambavyo wamekuwa wakijitolea kuleta maendeleo katika kata yao. 

Sambamba na hayo amewahimiza vijana kuendelea kujishughulusha na shughuli za kijamii ili kujipatia kipato hali itakayozidi kuwafanya waaminiwe na jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla, na kufuta dhana iliyozoeleka kuwa vijana mitaani ni wezi. 

Amesema iwapo katika bajeti ya mwaka 2024/2025  watapatiwa fungu kama walivyoomba, wanatarajia kujenga majengo ya ghorofa katika shule za sekondari  na msingi kwa sababu ya ufinyu wa maeneo kwa shule zilizoko mjini,

kuongeza matundu ya vyoo na ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari Ungalimited. 

Pia amebainisha jitihada mbalimbali zinazofanywa ikiwa ni pamoja na kutengeneza barabara katika kiwango cha lami, kuweka kwaru na marekebisho mengine, ambapo hali inaendelea kuwa nzuri kwa barabara zilizoko chini ya TARURA na hata zilizo nje ya TARURA matengenezo yanaendelea.

"Pia naishukuru Serikali yetu kwa maamuzi ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira katika Kata ya Kisongo ambapo mashindano ya AFCON yatafanyika hapa kwetu Mwaka 2027, naamini hatua hii itakuza uchumi wetu, barabara nyingi zitatengenezwa kwa kiwango cha lami, na kuongeza ajira kwa vijana wetu" Amesema Mahmoud. 

Amewakumbusha wananchi wa Kata ya Ungalimited kukosoa pale wanapogundua mambo hayapo sawa kwani ushirikiano wao wa mawazo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wao. 


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post