SHULE YA MSINGI LUBAGA MKOANI SHINYANGA IMESHIKA NAFASI YA 10 BORA MIAKA MINNE MFULULIZO KWA UFAULU, MFANYABIASHARA GILITU APATA TUZO YA HESHIMA

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lubaga Stella Lucas  Halimoja akimkabidhi cheti cha heshima mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited Bwana Gilitu Makula kwa lengo la kutambua mchango wake katika kuchochea maendeleo ya shule ya msingi Lubaga.

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Shule ya msingi Lubaga iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imempa cheti cha heshima mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited Bwana Gilitu Makula kwa kuchochea maendeleo na ustawi wa shule hiyo hali iliyosababisha kushika nafasi ya 10 bora ngazi ya Halmashauri kwa Miaka minne mfululizo.

Hayo yamebainishwa na Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lubaga STELLA LUCAS  HALIMOJA wakati  akisoma risala  kwenye hafla fupi ya kumpongeza na kutambua juhudi na mchango wa Mfanyabiashara huyo wa Mkoa wa Shinyanga Bwana Gilitu Makula katika mafanikio,maendeleo na ustawi wa shule hiyo.

Mwalimu Stella amesema kwa Miaka minne mfululizo shule hiyo imekuwa ikiongeza wastani wa ufaulu katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba,juhudi ambazo zimetokana pia na mchango wa wadau wa maendeleo akiwemo Mfanyabiashara Bwana Gilitu.

“Kwa Miaka minne mfululizo tumekuwa tukiongeza wastani wa ufaulu katika matokeo ya kitaifa ya mtihani wa darasa la saba PSLE ambapo Mwaka 2020 tulikuwa na watahiniwa 52 tulipata ufaulu wa wastani wa alama 182.6538, Mwaka 2021 tulikuwa na watahiniwa 52 pia tulipata ufaulu wa wastani wa alama 223.9231, Mwaka 2022 tulikuwa na watahiniwa 92 tulipata ufaulu wa wastani wa alama 201.6848 na Mwaka huu 2023 tulikuwa na watahiniwa 71 tumepata ufaulu wa wastani wa alama 237.7887”.amesema Mwalimu Stella

“Kwa upande wa mitihani ya upimaji wa darasa la nne kwa Miaka mitatu mfululizo 2020 hadi 2022 tumeweza kufaulisha kwa asilimia Mia moja (100) kwa Miaka yote hiyo shule yetu imekuwa miongoni mwa shule kumi (10) bora katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga”.amesema Mwalimu Stella

Amesema kufuatia hatua hiyo uongozi wa shule ya msingi Lubaga umeanzisha utaratibu wa kutambua na kuwapongeza wadau wanaochochea maendeleo ya shule hiyo ambapo mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited amepewa tuzo ya heshima kwa mchango wake shuleni hapo.

“Kwa sababu hiyo uongozi uliona umuhimu wa kuweka utamaduni wa kuwatambua na kuwapongeza wadau wanaoshiriki kuendeleza ustawi wa shule yetu wakiwemo wazazi, walimu, mashirika mbalimbali, viongozi wa chama na serikali kwa kadri ya nafasi na uwezo wetu nia ikiwa ni kuendelea kuwatia moyo na kuendeleza ushirikiano baina yao na shule”.

“Katika kikao hicho ilibainika umuhimu mkubwa wa kuanza kwa kutambua mchango wa mdau muhimu sana Bwana Gilitu Makula mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited ambaye amekuwa na mapenzi makubwa na ustawi wa shule yetu ambaye leo tunampa tuzo ya heshima kwa moyo wake wa upendo na uzalendo, mdau huyo hasubiri kuarifiwa wala kuombwa chochote mbali hujitolea muda wake kutembelea shule, kuongea na walimu na wazazi kupitia kamati ya shule katika maongezi ya kawaida kisha kubaini uhitaji”.

“Bwana Gilitu Makula amejitolea kwa moyo kujenga baadhi ya miundombinu yeye mwenyewe ama kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo kuweka huduma ya umeme shuleni, kupaka rangi sura ya shule, kuchangia chakula kwa wanafunzi waweze kusoma muda wa ziada, kuwapatia msaada was are za shule wanafunzi wa kiume wanaotoka kwenye familia zenye uhitaji na kwa sasa anakamilisha ujenzi wa ofisi ya walimu na ameahidi kutupatia mashine ya Photocopy ili kurahisisha uzalishaji wa majaribio kwa wanafunzi”.amesema Mwalimu Stella

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited Bwana Gilitu Makula ameshukuru  kupewa tuzo hiyo huku akiahidi kuendelea kujitolea ili kuchochea maendeleo ya shule hiyo.

Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Walimu wa shule ya msingi Lubaga kwa ushirikiano wao pamoja na juhudi wanazozifanya katika ufundishaji ambapo amewaomba kuendelea na juhudi hiyo ili kuleta matokeo chanya zaidi.

Aidha Bwana Gilitu amesema amekuwa akipata ushirikiano mzuri kwa walimu wa shule hiyo huku akiipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kufungua milango wadau kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya kamati ya shule ya msingi Lubaga Bwana John Myola amesema siri kubwa ya mafanikio hayo ni ushirikiano uliopo kati ya wazazi, walimu, serikali na wadau mbalimbali huku akimpongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited Bwana Gilitu Makula kwa ushiriki wake mzuri katika kutatua changamoto.

Mgeni rasmi  katika hafla hiyo afisa elimu elimu maalum sekondari Essau Nyeriga ambaye amemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga naye amempongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited Bwana Gilitu Makula kwa majitoleo yake katika sekta ya elimu ambapo amemuomba kuendelea na moyo huo wa kuisaidia serikali kufikia malengo yake.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Lubaga Mhe. Ruben ameomba ushirikiano uliopo uendelea kwa lengo la kuongeza zaidi ufaulu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Lubaga.

Shule ya msingi Lubaga iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ni kati ya  shule zilizoshika nafasi ya 10 bora ngazi ya Halmashauri kwa Miaka minne mfululizo, ambapo hali iliyochangiwa na juhudi na ushirikiano mzuri baina ya wadau na walimu ambapo hafla  hiyo imehudhuriwa na wazazi, walimu, watendaji pamoja na wenyeviti wa mitaa kata ya Lubaga Manispaa ya Shinyanga.

 

 

 
This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post