MBUNGE WA KISHAPU MHE. BUTONDO ASISITIZA KASHWASA KUTATUA HARAKA CHANGAMOTO YA UKOSEFU WA MAJI, RC MNDEME ATOA MAAGIZO.

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mbunge wa jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo amesema ni vyema Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) kutatua haraka changamoto ya kukatika kwa maji mara kwa mara ambapo hali hiyo inasababisha  usumbufu kwa watumiaji wa huduma hiyo majumbani na kwenye maeneo ya Biashara.

Mhe. Butondo ameyasema hayo leo kwenye kikao cha kawaida cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Shinyanga ambapo amesema katika Jimbo la Kishapu upatikanaji wa majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria yanayowezeshwa na KASHWASA yamekuwa yakitoka mara moja kwa wiki.

Ametumia nafasi hiyo kuisisitiza mamlaka ya KASHWASA kuhakikisha inatimiza wajibu katika kuwafikishia huduma bora ya maji wakazi wa Jimbo la Kishapu ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo mlipuko wa magongwa kama vile kipindupindu na magongwa mengine.

Mbunge wa wa jimbo la Kishapu Mhe. Butondo ameeleza kuwa siku za hivi karibuni amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kuwa ni usumbufu na kwamba imekuwa ikisababisha hatari katika uendeshaji wa shughuli za kibiashara ambazo zinategemea huduma ya maji.

“Jimbo la Kishapu kama tunaadhabu maana hatupati maji sawa sawa tatizo kubwa lililopo tunapata maji kwa wiki mara moja wakati mwingine wiki mbili hatujapata maji ya Ziwa victoria ile maana ya kumtoa mama ndoo kichwani tunaenda kuipoteza sasa hili KASHWASA ni lazima mseme tatizo kubwa hasa ni nini kwa sababu kama ni fedha mnafanya biashara na mnapata fedha, fedha ile mnapaswa kuirudisha ije kuhudumia miradi ya wananchi”.

‘Mimi na mkuu  wa Wilaya ya Kishapu tumewahi kuwatembelea KASHWASA ofisini kwenu ilikuwa ni Mwaka wa fedha uliopita mkaahidi mwaka wa fedha huu ambao tunao kwamba zingetengwa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mabomba ya maji ili mfanye ukarabati mkubwa lakini mpaka sasa mwaka unaelekea kuisha sasa pengine mgezungumza na sisi tukajua aidha ipo changamoto kwenye wizara ya maji”.amesema Mhe. Butondo

Baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao hicho akiwemo mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Paschal Patrobas Katambi na mganga mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Luzila John wameiomba Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) kuwa na utaratibu wa kutoa ratiba ya uhakika ili kuwawezesha watumiaji kuhifadhi maji ya kutosha,kuliko hivi sasa ambapo taarifa zinazotolewa zinakuwa hazieleweki.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amesema halidhishwi na mamlaka ya KASHWASA katika shughuli za ugawaji maji huku akiiagiza  kutatua changamoto hiyo kwa haraka ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.

Amesema serikali ya awamu wa sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha zaidi ya Bilioni mia moja kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji Mkoa wa Shinyanga.

RC Mndeme ameitaka KASHWASA kufuta ratiba ya mgao wa maji ambayo imetoka wakati changamoto ya  maji ikiendelea huku akiwahimiza kutatua haraka changamoto iliyopo.

Mkurugenzi mtendaji wa  KASHWASA mhandisi Patrick Nzamba amekili kuwepo kwa changamoto zilizosababisha mgao wa maji ambapo ameahidi kuendelea kushughulikia changamoto zilizopo ili kuondoa usumbufu unaojitokeza.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akiitaka KASHWASA kutatua changamoto ya ukosefu wa maji.

Mbunge wa jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo akiisisitiza KASHWASA kutatua changamoto ya kukatika maji mara kwa mara katika Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga.

Mbunge wa jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo akiisisitiza KASHWASA kutatua changamoto ya kukatika maji mara kwa mara katika Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga.

Mkurugenzi mtendaji wa  KASHWASA mhandisi Patrick Nzamba akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na viongozi mbalimbali kwenye kikao cha  kawaida cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Shinyanga.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi na katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Bi. Odilia Batimayo upande wa kulia wakiwa katika kikao cha kawaida cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Shinyanga.
This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post