SERIKALI YAFANIKIWA KUDHIBITI UGONJWA WA MARBURG ULIORIPOTIWA KAGERA

Na Mapuli Misalaba

Serikali imefanikiwa kudhibiti ugonjwa wa  MARBURG ulioripotiwa katika Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera kuwa jumla ya watu nane (8) walithibitika ambapo watano (5) kati yao walifariki na watatu (3) wanaendelea na matibabu katika vituo vya kutolea huduma.

 Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu hii  March 25, 2023 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera na kusema mpaka sasa hakuna visa vipya vya wagonjwa wala kifo kilichotokea.

 Waziri Ummy Mwalimu  amesema kuwa serikali imefanikiwa kudhibiti ugonjwa huo usisambae maeneo mengine Nchini na kwamba mpaka sasa jumla ya watu 205 wanafuatiliwa kwa karibu kwa kuwa walitangamana na wagonjwa au wahisiwa.

 “Niwatoe hofu wananchi kuwa Serikali imeudhibiti ugonjwa huu usisambae maeneo mengine nchini hadi sasa kama tulivyoeleza hatujapata wagonjwa au wahisiwa wengine nje ya kaya mbili zilizoripoti awali ambazo ni kata ya Maruku na Kanyangereko”.amesema Waziri Ummy

 “Hadi kufikia  tarehe 25 Machi, 2023, tumeendelea kushuhudia kwamba ugonjwa huu unadhibitiwa maana hatujapata wagonjwa wapya waliothibitika, licha ya kuendelea kupokea tetesi na wahisiwa kadhaa. Mfano, siku ya tarehe 22 Machi, 2023 tulipata wahisiwa watatu (3) na wote baada ya kuchukuliwa sampuli, wamekutwa hawana maambukizi.

 “Tumeongeza wataalam 6 wa afya ikiwemo daktari bingwa bobezi wa magonjwa ya Figo, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na wauguzi waliopata mafunzo maalumu kutoka maeneo mengine ili kusaidiana na wataalam wa Afya wa hapa Mkoani Kagera katika kuendela kutoa huduma kwa wagonjwa watatu waliopo katika vituo vyetu vilivyoandaliwa”. Amesema Ummy

 “Lakini tunaendelea kufuatilia watu waliotangamana kwa namna mbalimbali na wagonjwa au wahisiwa, ambapo hadi leo tuna jumla ya watu 205 tunaowafuatilia (contacts) kwa karibu kwa kuwa walitangamana na wagonjwa au wahisiwa watu hawa wote ni wanafamilia waliouguza wagonjwa na watumishi wa Afya waliohudumia wagonjwa watu hawa kwa mujibu wa taratibu za afya kuhusu udhibiti wa maambukizi, tunawafuatilia kuhusu mwenendo wa afya zao kwa kipindi cha siku 21 ili kujiridhisha endapo wataonyesha dalili za ugonjwa au la”.amesema Waziri wa Afya Mhe. Ummy

 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amefafanua namna ugonjwa huo unavyoambikizwa ikiwemo mkojo, damu, machozi, kutoka kwa wanyama, pamoja na kugusa majimaji ya mwili wa mtu mwenye ugonjwa huo.

 “ Ugonjwa wa Marburg huambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hususan kwa njia ya kugusa majimaji mfano mate, mkojo, damu, machozi au kinyesi kutoka kwa mtu aliyefariki kwa ugonjwa huu au kutoka kwa mtu mwenye maambukizi ya Virusi vya Marburg anayeonyesha dalili za ugonjwa huu vilevile, maambukizi yanaweza pia kutokea kutoka kwa wanyama hasa Popo, Tumbili na  Nyani na kwenda kwa binadamu iwapo mtu atakula au kugusa mizoga au wanyama walioambukizwa”.

 “Serikali pia imeimarisha ufuatiliaji wa visa na wahisiwa katika jamii yetu yote kwenye maeneo hatarishi ikiwemo visiwa vya Ziwa Victoria  ili kujihakikishia kuwa tunaendelea kuwa salama. Aidha tunaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu ugonjwa huu ikiwemo dalili na jinsi ya kujikinga”.amesema Mhe. Ummy

 “Timu za wataalam wetu wako maeneo mbalimbali ikiwemo pamoja na mipaka yetu ili kuimarisha zaidi udhibiti wa ugonjwa huu. Niwaombe ndugu zangu wana Bukoba na wanaKagera kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zaidi zitakazosaidia kuudhibiti ugonjwa kwa haraka zaidi”. Amesema Ummy Mwalimu

 Aidha Waziri huyo ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wote kuendelea kuzingatia Miongozo na Taratibu za Kuzuia na Kudhibiti Maambuzi zinazotolewa na wataalam wa Afya ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za ugonjwa huo kwa wakati.

 “Nawaomba muendelee kuzingatia Miongozo na Taratibu za Kuzuia na Kudhibiti Maambuzi (Infection Prevetion and Control) wakati wote wa kutoa huduma kwa wagonjwa ni matumaini yangu kwamba ugonjwa wowote wa kuambukiza hautawakuta kwa kuwashtukiza bali mtaubaini mapema na kuuzuia katika eneo moja na kutoa tiba stahiki”.

 “Hata hivyo nawaomba wananchi wote kuendelea kuzingatia njia za kujikinga na tahadhari dhidi ya ugonjwa huu aidha ninawaomba wananchi  kote nchini kufuatilia taarifa rasmi za mwenendo wa ugonjwa huu kutoka Wizara ya Afya na Mamlaka husika za Serikali sambamba na kutoa taarifa kwa Serikali kupitia Ofisi za Serikali za Vijij/Mitaa au Vitongoji  au kupiga simu namba 199 bila malipo endapo kuna mtu mwenye dalili zinazofanana na ugonjwa huu”.amesema Ummy

 Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Wadau mbalimbali inaendelea kudhibiti  maambukizi ya ugonjwa huu kwa kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo uimarishwaji wa elimu ya afya kwa umma na ushirikishwaji wa jamii, ufuatiliaji wa wagonjwa na wahisiwa, afua ya udhibiti wa magonjwa ambukizi yaani Infection Prevention and Control  sambamba na huduma za upimaji na tiba dhidi ya ugonjwa wa Marburg.

    Siku kumi (10) zimepita tangu tupate taarifa za ugonjwa wa Marburg katika kata za Maruku na Kanyangereko, Halmashauri ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera ambapo tarehe 21 Machi 2023 Waziri wa Afya Mhe. Ummy alitangaza rasmi kuhusu uwepo wa maambukizi ya Virusi vinavyosababisha Ugonjwa wa Marburg baada ya majibu ya uchunguzi wa kimaabara kuthibitisha uwepo wa Virusi hivyo. 

 Mtu mwenye maambukizi ya Virusi vya Marburg hawezi kuambukiza wengine kabla hajaonesha dalili za ugonjwa huu”.

 


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post