SIDO ARUSHA YAWAFUNDA WAMILIKI VIWANDA VIDOGO

 Na Magesa Magesa,Arusha

SHIRIKA la kuhudumia viwanda vidogo nchini (SIDO)Mkoani hapa, limewataka wamiliki wa viwanda vidogo mkoani hapa kuhakikisha kuwa wanakuwa wabunifu na kuzalisha bidhaa bora ili kukabiliana na ushindani wa kibiashara uliopo sasa.

Meneja wa SIDO Mkoani hapa Jalphary Donge aliyasema hayo jana Jijini hapa, alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wamiliki na wakurugenzi wa viwanda vidogo yaliyofanyika katika ofisi za shirika hilo.

“Msifanye biashara kwa uzoefu hakikisheni mnakuwa wabunifu, zalisheni bidhaa bora zenye viwango vya hali ya juu kwani kwa sasa kumekuwa na ushindani mkubwa sana pindi bidhaa zifikapo sokoni”alisisitiza Donge

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wamiliki na wakurugenzi hao juu utoaji wa huduma za maendeleo ya biashara(BDS)ambayo yalifadhiliwa na UNICO-JICA kwa kushirikiana na SIDO Mkoani hapa.

Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo,Edward Rwegoshora kutoka Shirika la kubadilisha na kuboresha maisha ya watanzania(STAWI)aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha kuwa wanazingatia yale yote waliyofundishwa na waende wakayafanyie kazi kwa vitendo.

 Aliwataka kuhakikisha kuwa wanafanya utafiti ili kupata uzoefu na kupima utayari wa upokeaji wa huduma za maendeleo ya biashara lengo likiwa ni kuendeleza biashara zao na kuvutia wateja wengi zaidi.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Diana Mamuya kutoka
kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Anna aliwapongeza SIDO kwa kuandaa mafunzo hayo  na kusema kuwa yamekuja kwa wakati muafaka na kushauri muda uongezwe katika kupatiwa mafunzo hayo


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post