VIONGOZI WASISITIZWA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA ZA UMMA

Afisa Maendeleo ya Jamii Shaban Manyama, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.

 

Na Zulfa Mfinanga, Arusha.


Wananchi wa Mtaa wa Mlimani Kata ya Muriet Jijini Arusha wametakiwa kuhakikisha wanatunza mradi wa shule mpya ya sekondari inayoendelea kujengwa  ikiwa ni pamoja na kutumia fedha zilizotolewa kwa lengo lililokusudiwa.



Akizungumza kwenye kikao cha majadiliano na wananchi wa eneo hilo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Arusha Shaban Manyam aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji amesema njia moja wapo ya kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa ni pamoja na kuwasomea wananchi mapato na matumiazi ya mradi huo kila baada ya wiki mbili.



Amesema kwa kuwa ujenzi huo ni wa kutumia force account wanatarajia kuona masuala ya manunuzi kwa kufuata bei ya soko na siyo bei ya mkandarasi kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha.



“Niwatake Kamati zilizopo na viongozi wa Kata msimamie kwa ufanisi ujenzi huu kwa weledi na uzalendo wa hali ya juu ili ukamilike kwa wakati na kwa gharama iliyotengwa, hatutaki bei ambazo hazituletei tija, tumieni Force account, na muwasomee wananchi mapato na matumizi kila mara” Alisema Manyama.



Manyama amesema mradi huo umetolewa mahsusi nchi nzima kwa Kata ambao hazina shule lengo likiwa ni kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi ili kuwasaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule kwa kuzingatia kuwa Kata hiyo ina shule moja tu ya sekondari.



Afisa Elimu Taaluma Sekondari Mwl. Fidea Makwinje
Afisa Elimu, Kilimo na Mazingira Caroline Kiwori



Amesema mradi huo wa shule utajengwa kwa mtindo wa ghorofa umetengewa kiasi cha shilingi milioni 600 na tayari kiasi cha shilingi milioni 470 zimeshatolewa na kuongeza kusema kuwa usimamizi bora wa mradi huo utapelekea kupewa fedha nyingine kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini kinyume na hapo hawatapata fedha nyingine.



Naye Afisa Elimu Taaluma Sekondari Fidea Makwinje aliwataka wananchi hao kuutunza mradi huo kwani umeletwa kwa ajili ya watoto wao huku mzee wa kimila Tobiko Kivoini kwa niaba ya wananchi wenzake akimshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo licha ya kukaa madarakani kwa kipindi kifupi.



Afisa Elimu Kilimo na Mazingira ambaye pia ni msimamizi wa mradi huo, Caroline Kiwori pamoja Afisa Mazingira kutoka Jiji la Arusha Sigfrid Mbuya wamezitaka kamati zinazosimamia mradi huo kuhakikisha wanafuata maelelekezo yote muhimu yaliyotolewa na Benki ya Dunia.



Walitaja maelekezo hayo kuwa ni  pamoja na kukakikisha wafanyakazi katika mradi huo wanafanya kazi katika mazingira safi na salama kwa kuvaa vifaa vya usalama kama vile buti, kofia ngumu, vyoo, kupata chakula na maji katika mazingira safi na salama.



Fatuma Amir, Mratibu wa mradi

Maelekezo mengine ni kuepuka ajira za watoto, ajira zote zizitangie usawa wa kijinsia , vibarua na wafanyakazi wote wawe na mikataba ya kazi pamoja na kushughulikia kwa wakati matatizo yoyote yatakayojitokeza.



Mratibu wa mradi huo Fatuma Amir pamoja na Mtendaji wa Kata ya Muriet Lucy Sungi wamesema wamepokea maelezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wananchi wa eneno hilo bega kwa bega ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post