DKT PIMA AKATAZA SIASA KWA WAANDISHI WA ANWANI ZA MAKAZI ARUSHA

vijana watakaokuwa wakiandikisha anwani za makazi katika kata 20 za jiji la Arusha wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Jiji la   Arusha Dkt John Pima (Hayupo pichani), alipokuwa akizundua mafunzo ya siku moja kwa vijana hao yanayoendelea katika shule ya mchepuo wa kiingereza ya Arusha School Arusha 
Msimamizi wa kata sita za Jiji la Arusha, Ernesta Moshi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo ya namna ya utekelezaji wa zoezi hilo kwa vijana watakaokwenda kufanya zoezi hilo katika kata 20 za jiji la Arusha

 

Na Seif Mangwangi

MKURUGENZI wa Jiji la Arusha Dkt John Pima amewataka vijana wanaosimamia zoezi la anwani za makazi kutojihusisha na mambo ya kisiasa katika maeneo watakayokuwa wanafanyia kazi kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha maadili ya utumishi.


Akizungumza na kundi la vijana walioteuliwa kwaajili ya kuweka anwani za makazi (post code), sanjari na kubainisha na kuweka alama na majina ya mitaa katika kata 20 zilizosalia za Jiji la Arusha , Dkt Pima amesema zoezi hilo ni nyeti na linahitaji uangalifu wa hali ya juu. Tayari Jiji hilo linaendelea na zoezi hilo katika kata tano za awali.


“Nimekuja hapa kufungua mafunzo yenu lakini pia kuwaeleza mambo machache ambayo tunayatarajia kutoka kwenu, sitarajii kusikia miongoni mwenu mmejihusisha na mambo ya kisiasa, lolote mtakalolisikia toeni taarifa kwa msimamizi wako,”amesema.


Amesema vijana hao wanapaswa kujua kuwa kazi ya Serikali ni kazi ya siri kubwa na hivyo hatarajii mambo yanayohusika na siri za zoezi hilo yatoke nje ya viongozi wanaosimamia zoezi hilo au yeye mkurugenzi.


Dkt Pima amewataka vijana hao kufanyakazi hiyo kwa bidii ili kuhakikisha linakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa na Serikali na kwamba endapo watakutana na vikwazo vyovyote watoe taarifa mapema kwa maafisa wanaowasimamia.


“Tunatarajia zoezi hili la awali litaisha ndani ya wiki mbili kuanzia kesho Februari 22, 2022, baada ya hapo mtaendelea na zoezi lingine gumu zaidi ambalo ni kuweka alama ambapo hatua hii umakini zaidi tena unahitajika na ninaamini kwa jinsi ninavyowaona mnaweza kufanyakazi vizuri sana,”anasema.


Kwa mujibu wa Mkurugenzi Dkt Pima Jiji la Arusha linatarajia kumaliza zoezi hilo Machi mwaka huu, huku kitaifa zoezi hilo likitarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Mei 2022.  


Kwa upande wake msimamizi wa zoezi hilo katika kata sita ndani ya Jiji la Arusha Ernesta Moshi amesema amepokea maelekezo ya Mkurugenzi kuhusiana na maadili katika kazi hiyo na ameshatoa maelekezo kwa vijana wanaoenda kutekeleza zoezi hilo kuwa makini.



This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post