SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA POSTA NCHINI

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Naibu Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ametaka wadau wa Sekta ya Posta nchini kushirikiana katika kuhakikisha utoaji wa huduma zenye tija kwa wananchi 


Hayo ameyasema tarehe 18 Januari, 2022, alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Posta Afrika (PAPU) ambapo amemwakilisha Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye


Mhe. Kundo amesema kuwa Serikali inatambua juhudi ambazo Sekta ya Posta nchini inafanya katika kuendana na maendeleo ya teknolojia ambayo yamekuwa chachu ya kubadili mifumo mbalimbali ya kiutendaji ndani ya Shirika la Posta


“Serikali inatambua juhudi ambazo Sekta ya Posta inafanya kuelekea mageuzi yanayoletwa na teknolojia na kubadili mifumo mbalimbali ya kiutendaji ndani ya Shirika la Posta”. Alisema Mhe. Kundo


Aidha, Mhe.  Kundo ameongeza kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za posta na kituo Cha kutegemeza TEHAMA kwa nchi zinazoongea kiingereza  kipo nchini Tanzania hivyo uwepo wa Makao Makuu ya Umoja wa Posta (PAPU) Jijini Arusha unaimairisha umuhimu wa ufanisi wa utoaji huduma za posta katika nchi mbalimbali.


Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika, Chief Sifundo Moyo alisema Umoja huo unazidi kukua kwa kuboresha huduma mbalimbali za posta ikiwemo kushirikishana mbinu za mashirika ya posta kutokana na ukuaji wa teknolojia hususan teknolojia za simu na usafirishaji wa mizigo kupitia posta cargo


Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari amesema, TCRA itaendelea kusimamia na kuunga mkono jitihada za Sekta ya Posta nchini katika kukuza mawasiliano yatakayoleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.


Naye PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania,Macrice Mbodo amesema kuwa katika mkakati wa nane Shirika hilo limeweka vipaumbele katika huduma za usafirishaji, huduma za fedha na uwakala, biashara mtandao, uimarishaji wa vituo vya Huduma Pamoja na mifumo ya TEHAMA .


Nao wadau wa Posta wameiomba Serikali kuondoa mkanganyiko wa ushuru wa forodha ambao umekuwa ukisababisha wafanyabishara  kutoingiza bidhaa zao nchini na  badala yake kutumia nchi ya Kenya kuingiza mizigo na kuisafirisha kuja nchini kwa njia ya biashara mtandao kwani kutokana na ushuru wa forodha kutoeleweka katika bidhaa wanazoagiza nje ya nchi kuja nchini kampuni mbalimbali za usafirishaji zinashindwa kuelewana na wateja na hatimaye wateja kususia mizigo yao na kampuni kupata hasara.


Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu "Kuimarisha Ushirikiano na Watoa Huduma Wengine wa Sekta ya Posta Afrika” yalihudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) Sifundo Chief Moyo na Msaidizi wake Jessica Hope Ssengooba, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Said Mtanda aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabir Bakari, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba, Katibu Mtendaji wa TCRA CCC Mary Msuya, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara Dkt Jim Yonazi na wadau mbalimbali wa Sekta za Mawasiliano nchini, ikiwemo Chama Cha watoa huduma za Posta nchini.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post