Waethiopia 51 wakamatwa Kondoa

 Na Rhoda Simba Dodoma.


JESHI la Polisi jijini hapa limewatia mbaroni wahamiaji haramu 51 raia wa Ethiopia na watu wawili raia wa Tanzania waliokuwa wakisafirishwa katika gari la mizigo wakitokea kanda ya kaskazini kuelekea Mikoa ya Kusini.

 

Akizungumza na waandishi wa habari  leo Disemba 28 jijini hapa kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma SACP Onesmo Lyanga amesema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa tarafa ya Bereko Wilaya ya Kondoa wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T.593 AUE aina ya fuso likiendeshwa na Ignas Mgosi (23) mkazi wa mafinga akisaidiwa na Jafari Idd (39) mkazi wa Arusha.

 

 

“Askari walipekua gari  hilo  na kuwakamata wahamiaji hao raia wa Ethiopia wakitokea Moshi Kilimanjaro kwenda Iringa mbinu iliyotumika ni kuwaficha kwa turubai kiini cha  tukio ni kukosa uzalendo wa nchi na tamaa mbaya ya kujiptia kipato  isivyo halali” amesema  kamanda Lyanga.

 

 

 

Aidha ametoa wito kwa vijana wa kitanzania na madereva na wamiliki wa magari kuwa waache tamaa ya kufanya vitendo vya uhalifu kwa kuwa uhalifu haulipi.

 

 “Kwa mujibu wa sheria ya nchi  kifungu 46 (1) (a) – (g) cha sheria ya uhamiaji sura  ya 54 siyo tu watuhumiwa kufikishwa  mahakamani na kupata hukumu ya kifungo bali ni pamoja na gari lililohusika kufirisiwa na wamiliki kupata umasikini”amesema  Lyanga

 

Kwa upande wake Mrakibu Mwandamizi wa uhamiaji Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni kaimu Afisa uhamiaji  Adam Mkuyu amesema wamejipanga kila kona kuhakikisha hakuna mhamiaji anaingia kinyemela.

 

“Sisi uhamiaji tumejipanga kila sehemu kuhakikisha  vitendo hivi vya uhamiaji haramu  tunavipiga vita vikali lakini pia nitoe wito kwa wenzetu ambao wanahitaji kuhamia nchini kwetu wafate sheria na kanuni za uhamiaji”amesema Mkuyu.

 

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post