TANROADS YASISITIZA UTUNZAJI MIUNDOMBINU YA BARABARA

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Athumani Kihamia

Na Mwandishi Wetu, Arusha

WAKALA ya Barabara Tanzania (TANROADS) Novemba 15, 2021, imeendelea kufanya Warsha kwa Wadau wa Sekta ya Usafirishaji kuhusu Sheria ya Afrika Mashariki ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za Mwaka 2018.


Warsha hiyo imefanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha na kuwakutanisha wadau wa sekta ya usafirishaji kutoka Mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha.


Arusha ni Mkoa wa 12, kuwakutanisha wadau wa sekta ya usafirishaji kwa ajili ya warsha hiyo inayohusisha jumla ya Mikoa wenyeji 13 ya Tanzania bara.


Akizungumza wakati wa kuhitimisha warsha hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Athuman Kihamia, amesema uzingatiwaji wa sheria hiyo utapelekea kulindwa kwa miundombinu ya barabara.


Amesema serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa barabara hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuitunza.


Dkt. Kihamia amebainisha kuwa nyenzo kuu za maendeleo katika taifa lolote Duniani ni elimu na miundombinu ya barabara hivyo jukumu la kuitunza linapaswa kutiliwa mkazo.


“Ikishakuwepo miundombinu hata bei za mazao zinapungua na gharama za maisha zinakuwa chini, kwa kuwa uendeshaji wa shughuli mbalimbali unakuwa rahisi,” ameeleza.


Amewataka wadau wa sekta ya usafirishaji kuwa mabalozi wazuri wa elimu hiyo, kwa kuhakikisha wanaifikisha na inatumika na wadau wote.


Aidha, ametoa wito kwa TANROADS kutumia mbinu mbalimbali kufikisha elimu hiyo kwa wadau wa sekta ya usafirishaji ikiwemo kutengeneza vipeperushi na kutumia vyombo vya habari.


Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Arusha, Mratibu wa Polisi Solomon Mwangamilo, amesema miundombinu hasa ya barabara huigusa moja kwa moja jamii.


“Tunatambua kwamba serikali inatumia gharama kubwa kujenga barabara, sasa kila mwananchi ana jukumu la kuzitunza kwa kadri iwezekanavyo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu katika matumizi yake,” amesema.


Amesema kitendo cha gari kuzidisha uzito wa mizigo kinasababisha uharibifu wa barabara, ambao hatimaye unaigharimu serikali kufanya ukarabati.


Amesisitiza kwamba, warsha hiyo itajenga uelewa kwa wasafirishaji kuhusu uzingatiaji wa uzito wa mizigo wanayobeba katika magari.


Naye, Kaimu Meneja wa Shughuli za Mizani kutoka TANROADS, Eng. Japhet Kivuyo, amefafanua changamoto ya baadhi ya magari kuonekana yamezidi katika mzani mmoja na mwingine kuonekana sawa, akisema hiyo inatokana na kutozingatia asilimia tano iliyowekwa na sheria kufidia kucheza au kuhama kwa mzigo.


“Kwa kawaida tunajua barabara zetu sio kioo, unakuta zina matuta ambayo huweza kusababisha mzigo kuhama kutoka mtaimbo mmoja kwenda mwingine, hivyo sheria hii imeweka asilimia tano zinazopaswa kuachwa na msafirishaji kufidia hilo,” amesema.


Amesema kinachosababisha malalamiko mengi katika hilo, ni baadhi ya wasafirishaji kupakia mzigo bila kuacha asilimia tano zilizotajwa na sheria kufidia kuhama au kucheza kwa mzigo.


Akizungumzia warsha hiyo, Mtaalamu kutoka Kitengo cha Mizani TANROADS Makao Makuu, Eng. Vicent Tarmo, amesema warsha hiyo ni muendelezo kwa kuwa kila siku zinaanzishwa kampuni mpya za usafirishaji. 


Amefafanua pamoja na mambo mengine wadau wa sekta ya usafirishaji katika warsha hizo huelimishwa kuhusu taratibu za upimaji wa magari na athari za kuzidisha uzito. 


Amesema pia wameelimishwa kuhusu sheria inayosimamia mizigo mipana na maalumu. 


Ameongeza kuhusu sababu ya Mizani kuonyesha uzito tofauti kwa Gari moja kwamba, inatokana baadhi ya madereva kufanya chochote kinachoongeza uzito bila wenyewe kujua kwamba kinaweza kuleta mabadiliko katika uzito waliobeba.


Amesema hali hiyo hujitokeza iwapo dereva ameongeza mzigo, abiria au mafuta akiwa njiani, pia kuchezea Busta ambayo husababisha gari kubadilika kipimo kutoka kituo kimoja cha mzani hadi kingine. 


Ameitaja asilimia tano iliyowekwa kisheria kufidia changamoto zote barabarani ni miongoni mwa sababu za hilo, kwani wasafirishaji huitumia kama sehemu ya kubebea mzigo. Locken Masawe ni Katibu wa Wasafirishaji Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, amesema warsha hiyo imewapa mwanga wa kufahamu mengi wasiyoyajua.


Aliipongeza TANROADS kwa kuandaa warsha hiyo na kuongeza kuwa hatua hiyo inadhihirisha ukweli kwamba, kuna muelekeo mzuri wa ushirikiano baina ya wakala huo na wadau wa sekta ya usafirishaji.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post