*Polisi Goba, wajeruhi kwa kipigo, majeruhi yuko ICU MOI, anapumulia mashine, ndugu waelezwa kupona kwake utakuwa muujiza wa Mungu*

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Ramadhani Kingai
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Muliro J. muliro


 *Majeruhi aomba IGP Sirro afikishiwe salamu

Na Mwandishi Wetu

Jumatano, November 10, 2021, Polisi Goba walidaiwa kumkamata Issa Kassim (20), nyumbani kwao huko Goba kwa madai kwamba ameuziwa TV ya wizi, tukio ambalo mtuhumiwa alikana kulitenda.

 

Baada ya kumkamata mashuhuda wa tukio hilo walidai askari hao waliondoka naye wakidai wanampeleka kituo cha polisi Goba, lakini kabla ya kufika huko kituoni walimuomba awapigie simu ndugu zake waweze kumuokoa.

 

Mtuhumiwa (Issa Kassim), alipiga simu kwa mama yake akazungumza na mmoja wa polisi hao aliyefahamika kwa jina moja la Majuto.

 

Askari huyo wa jeshi la polisi kituo cha Goba, katika mazungumzo na Mama wa mtuhumiwa huyo inadaiwa alimuomba atume Sh.800,000 ili kijana wake waliyemshikilia kwa tuhuma ya kununua TV ya wizi waweze kumuachia.

 

Mama wa mtuhumiwa aliomba apunguziwe dau hilo, badala ya kuwapatia Tsh 800, 000 atume Tsh500,000, na  ombi lake lilikubaliwa na kutakiwa atume kiasi hicho cha fedha.

 

Wakati biashara hiyo ikiwa kwenye mazungumzo, mtuhumiwa issa ambaye alikuwa akisikia mazungumzo hayo alimzuia mama yake kuwatumia polisi hao fedha yoyote akidai hajatenda kosa lolote, anasingiziwa tu.

 

Baada ya mtuhumiwa huyo kuzuia fedha kutumwa kwa polisi hao,  polisi hao wakiongozwa na Majuto, na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Paul walidaiwa kumpiga sana, hasa maeneo ya kichwa kwa kutumia nyaya ngumu wakidai ni jeuri anazuia wao wasitumiwe fedha ili aachiwe.

 

Mashuhuda walidai baadaye tena, akiwa tayari amepokea kipigo cha kutosha kutoka kwa polisi hao, alitakiwa kumpigia simu ndugu yake mwingine mwenye uwezo kifedha ili atume fedha hiyo aweze kuachiwa. 

 

Alipigiwa simu binamu wa mtuhumiwa huyo aitwaye Tusekile Shadrack, ambaye alielezwa tukio hilo, na kutakiwa na afande Majuto, wa jeshi la polisi Goba atume fedha sh 800, 000 ili ndugu yake aweze kuachiwa na kufutiwa kesi inayo mkabili. 

 

Ndugu huyo wa mtuhumiwa ilidaiwa alimuomba polisi Majuto ampe namba yake ya simu amtumie fedha hiyo, aligoma kutoa namba yake, akamtaka atume kwenye simu ya mtuhumiwa au apewe namba ya wakala atoe kupitia huko, ilishindikana, fedha haikutumwa, mtuhumiwa kwa mara nyingine alimzuia asitume chochote sababu yeye anasingiziwa tu, hajatenda kosa hilo.


Alhamisi, November 11, 2021, asubuhi, Afande Majuto ilidaiwa alimpigia simu Mama wa mtuhumiwa akimtaka afike Hospitali ya Mwananyamala haraka, hali ya mwanaye ni mbaya.

 

Mama huyo wa mtuhumiwa aliongozana na Tusekile binamu wa Issa kwenda Mwananyamala Hospitali, walipofika kweli walimkuta mtoto wao taabani lakini, aliweza kuongea kwa shida sana na kuwasimulia mkasa mzima uliomkuta.

 

"Nimepigwa sana, sidhani kama nitapona, niombeeni sana kwa Mungu, nimeumizwa, nakufa bila hatia yoyote, polisi wakiongozwa na Majuto,  wamenitesa na wamenipiga kipigo kikali  wananiua eti kwa sababu nimewakosesha fedha za dhuruma walizotaka kuzipokea kutoka kwenu ndugu zangu, niombeeni, nami naomba, Mungu atanilipia" alisema Issa ambaye alikuwa akiongea kwa tabu akiwa wodini katika hospitali ya Mwananyamala.

 

"Cha ajabu, yule mwizi waliyedai ameniuzia TV ya wizi aliachiwa, hakufika hata kituo cha polisi, aliambiwa tukiwa njiani tuna karibia kituo cha Goba atambae, nakufa, nifikishieni salaam zangu kwa IGP Sirro, askari wake wanawatesa raia, wanawaua kwa kuwapiga wakitaka walipwe pesa kwa makosa ya kutengenezewa ili wapate fedha ya dhuluma, nakuacha mama, niombee kwa Mungu" aliongea Issa kwa majonzi makubwa huku akiwa hoi hospitalini hapo.

 

Katika hospitali ya Mwananyamala alifanyiwa kipimo cha cit-scan na MRI kichwani, wakadai mishipa ya mfumo wa fahamu kichwani imeathiriwa pakubwa, damu nyingi imevia, imeganda na kuikandamiza mishipa hiyo kwenye Ubongo.

 

Kutokana na hali yake kuendelea kuwa mbaya na kuanza kushindwa kuongea ilibidi haraka sana ahamishiwe MOI, ambapo alipokelewa na yuko ICU.

Kwa mujibu wa binamu wa Issa, Tusekile, maelezo ya madaktari bingwa wa MOI wa mifumo ya fahamu ya kichwa(Neurosurgery) wanaomhudumia, wamesema kupona kwake ni asilimia moja, muujiza tu wa Mungu ndio unasubiriwa.!


"Ndugu tumekata tamaa, hivyo tunaomba msaada wa kisheria na ushauri,"alisema Tusekile.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai alipoulizwa kuhusiana na tukio hili alidai kulisikia na kwamba ofisi yake inaendelea kufuatilia ili kujua ukweli wake na itatoa taarifa rasmi baada ya kubaini ukweli wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Novemba16, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Jumanne Muliro amesema askari wake wanachunguza tukio hilo na watakaobainika watashtakiwa kwa mujibu wa sheria.

"Tumepokea malalamiko kutoka kwa wazazi wa mtuhumiwa mmoja anayejulikana kwa jina la Issa aliyekuwa akituhumiwa kwa wizi wa TV ambaye anadaiwa kupigwa na askari wetu wa kituo cha Goba, tunafanya uchunguzi kuhusu tukio zima, na vitendo vya rushwa, tukibaini ukweli hatua kali zitachukuliwa dhidi ya askari wetu,"amesema Kamanda Muliro.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post