NAIBU KATIBU MKUU MALIASILI NA UTALII AIPONGEZA TFS*


Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Ludovic James Nduhiye ameupongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS kwa namna ambavyo wakala huo ulivyofanya kazi kubwa katika kuhakikisha uwepo wa usimamizi madhubuti, wenye ufanisi na tija wa rasilimali za misitu na nyuki nchini.

Nduhiye alitoa pongezi hizo katika mkutano wake maalum wa kwanza na menejimenti na watumishi wa TFS uliofanyika Novemba 18, 2021 makao makuu ya wakala huo jijini Dar es Salaam.

Nduhiye alisema TFS inafanya kazi kubwa na imekuwa na mafanikio mengi katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na kusisitiza kuwa ukiangalia tatizo la mazingira na misitu lilivyo nchini unaweza usione kazi kubwa iliyofanywa na TFS.

 “Ukiangalia tatizo la mazingira nchini, usipokuwa makini unaweza ukaangalia tu changamoto iliyopo ukashindwa kuona kazi inayofanywa na TFS ya upandaji miti na  usimamizi endelevu wa rasilimali za taifa za misitu na nyuki, wakati mwingine unaweza kusema hizi ni siasa lakini uko Ushahidi wa twakwimu, 

“Juzi nilikuwa kwenye Kongamano la Uwekezaji Iringa nikiwa pale niliambiwa TFS mmepanda zaidi ya hekta 117,000 lakini ushahidi wa pili ni namna mnavyochangia kwenye maduhuli ya Serikali kupitia udhibiti na usimamizi mzuri wa sekta ya misitu, kwa hili TFS mnasitahili kutembea kifua mbele, mjiamini na mhakikishe kwamba majukumu mliopewa mnaendelea kuyatekeleza na kuyafanikisha,” alisema Nduhiye.

Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo alimuhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa licha ya kukumbwa na changamoto ya kukinzana kisekta Wakala huo utaendelea kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi endelevu wa rasilimali za taifa za misitu na nyuki ili kuchangia kikamilifu mahitaji ya kijamii, kiuchumi, ki-ikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho. 

“Ili kuondoa kukinzana kisekta tWakala umeandaa Andiko (Concept Note) la kuomba kuwa Mamlaka na tumeliwasilisha kwa mamlaka husika, tunaamini tukiwa na mamlaka ya Misitu na Nyuki itatusaidia kuwa na mamlaka ya kudhibiti sekta nyingine na kuondoa changamoto ya mawasiliano baina ya sekta moja na nyingine iwe ya kisheria ama utendaji wa kawaida,” alisema Kamishna Prof. Silayo.

Aidha, Kamishna huyo wa Uhifadhi aliongeza kuwa hali ilivyo sasa kuna upanuaji mkubwa wa mashamba ya kilimo na kwa bahati mbaya unaposikia kuna ardhi haitumiki vizuri kwenye kilimo basi inafahamika ardhi hiyo ni ile yenye misitu  na hivyo kuchochea uharibifu mkubwa wa misitu nchini na hivyo kwa kuanzishwa mamlaka tatizo hilo linakwenda kuisha.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post