Nasha kuzikwa Jumamosi Oktoba 2,2021 nyumbani kwake Ngorongoro

William Tate Ole Nasha

 Na Dotto Kwilasa - Dodoma

Serikali inaendelea kuungana na Watanzania wengine kuomboleza msiba wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Mhe. William Tate Ole Nasha ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ngorogoro mkoani Arusha ambaye umauti ulimkuta usiku wa kuamkia jana (Septemba 27,2021)nyumbani kwake maeneo ya Medeli Jijini Dodoma.

Akitoa taarifa ya Serikali,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi , Ajira na Watu Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema bado wanaendelea na vikao vya maandalizi ya maziko ya kitaifa huku akieleza kuwa marehemu Ole Nasha atazikwa Jumamosi,Oktoba 2 mwaka huu kijijini kwake kwa matakwa ya familia yake.

"Kesho siku ya Alhamisi tutafanya buriani ya kitaifa itakayohusisha viongozi wote katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania majira ya saa 5 asubuhi,kwa sasa tunaendelea na vikao vya ndani kati ya Ofisi ya Bunge na sehemu alikokuwa anaabudu marehemu kiimani ili kuona namna tutakavyompa heshima ya mwisho,"amesema Mhagama.

Aidha ameeleza kuwa baada ya mazungumzo yote Marehemu Ole Nasha atapewa heshima za mwisho kisha kuanza safari ya kuelekea kijijini kwake Arusha ambako atapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele siku ya Jumamosi.

"Ijumaa na Jumamosi ndiyo siku ambazo zitakuwa za maziko kijijini kwake,hayo ndiyo maamuzi ya kikao chetu cha awali, tutakaa tena saa kumi jioni kuona kama kuna jambo lingine jipya tutawajulisha,kwa sasa ni hayo tu,"amesisitiza Waziri huyo.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na familia ya marehemu Ole Nasha inaendelea kufanya mazungumzo pia na Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho kimemlea ili kufanikisha maandalizi yote muhimu kuanzia hatua za awali hadi mwisho wa maziko.

Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amewashukuru watanzania kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kipindi hiki cha maombolezo huku akiwataka kuendelea kuwa watulivu.

Kwa upande wake msemaji wa familia Edward Porokwa ameishukuru Serikaki na Chama Cha Mapinduzi kwa kuwapa ushirikiano tangu msiba ulipotokea na kwamba familia kwa ujumla imefarijika.

"Tumefarijika sana,Serikali imekuwa bega kwa bega na sisi tangu siku yabkwanza tulipo pokea taarifa za msiba wa ndugu yetu,jambo hili limetupa faraja ,"amesema Polokwa.

Mhe.William ole Nasha alizaliwa mwaka 1972 mkoani Arusha ambapo katika uhai wake ameitumikia Serikali katika nyanja mbalimbali ambapo hadi umauti unamkuta alikuwa akitumikia  nafasi ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post