KAULI YA RAIS MATIBABU YA CORONA YAWAIBUA WAGANGA TIBA ASILI

Dawa za mitishamba zikiwa tayari kutumiwa 
majani ya aina mbalimbali za miti iliyokuwa ikitumiwa kujifukizia wakati wa ugonjwa wa corona 
Mganga wa tiba asili akiwa na dawa zake za asili pembeni

 -WATINGA KWA MKEMIA MKUU WA SERIKALI KUTHIBISHA DAWA YA CORONA

-WATAMBA WALIIWEZA 'SURUA' CORONA INATIBIKA BILA TATIZO

Na Mwandishi Wetu, Arusha

AGIZO alilolitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli la kutaka dawa za asili zianze kuruhusiwa kuuzwa nchini, limeanza kuzaa matunda baada ya waganga wa jadi na  tiba za asili kuanza usajili wa dawa zao.

Wakizungumza juzi jijini hapa wakiwa katika harakati za kutafuta usajili wa dawa zao, katika maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kanda ya kaskazini, baadhi ya waganga wa tiba za asili kutoka maeneo mbalimbali kanda ya kaskazini walipongeza maamuzi ya Rais Dkt.Magufuli ya kuruhusu matumizi ya dawa zao.

Hata hivyo alisema kauli hiyo imechelewa kwa kuwa ni miaka mingi wao kama waganga wa tiba za asili wamekuwa wakitibia wagonjwa kwa kutumia dawa za asili za mizizi, majani na matunda na wagonjwa kupona.

Walisema kuwa ugonjwa wa corona (Covid -19), ambao umeendelea kuua maelfu ya watu duniani, dawa yake ipo miongoni mwa dawa ambazo wamekuwa wakizitumia kutibia wagonjwa wao na kwamba kupitia dawa hizo wagonjwa waliogundulika nchini waliweza kupona.

“Tunamshukuru sana Rais Dkt Magufuli kwa kutambua umuhimu na ubora wa dawa za asili, wakati janga la Corona lilivyoingia alisimama kidete na kutoa msimamo dhabiti kuhusu matumizi ya dawa za asili kwa kunywa na kujifukiza, na kweli tulipona,”alisema Dkt Daudi Nyaki, Mkurugenzi mkuu wa Chama  waganga wa tiba asili nchini (CHAWATIATA).

Rais Dkt John Pombe Magufuli akizindua bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu 2020, na yeye kuibuka mshindi aliziagiza mamlaka husika za dawa kuweka utaratibu wa dawa za asili kuanza kuruhusiwa rasmi nchini kama dawa zinazoweza kutibu magonjwa mbalimbali baada ya kufanyia uchunguzi na kuthibitishwa.

Kwa mujibu wa Dkt Nyaki baada ya kusikia tangazo la Mheshimiwa Rais baadhi ya waganga wa tiba asili kupitia chama chao walijikusanya na kukusanya dawa za asili ambazo wanaamini zinatibia ugonjwa wa Corona na kupeleka kwa mkemia mkuu wa Serikali.

 Mkurugenzi mkuu wa Chama hicho,Cha Chawatiata (T) Daud Nyaki,anasema dawa hizo wamezipeleka kwa mkemia mkuu wa serikali ili kujiridhisha na kuona kiwango cha ubora wake na uwezo wa kutibu kwa sababu ni mkusanyiko na mchanganyiko wa miti mbalimbali .

Anasema wataalamu hao wamekubaliana kupitia Chama chao kwamba kila mtaalam wa tiba asili awasilishe dawa zake kabla ya kuzitumia ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza jambo ambalo wasingependa kuliona.

“ Baada ya kusikia tangazo la Rais kila mmoja alichuma majani, kuchimba mizizi ya miti na magome yake na kisha kutoka na mzigo wa kutosha ambao wanaamini kuwa ni tiba tosha ya ugonjwa wa Corona, na hakika tiba hii ni sahihi kabisa, tunaamini mkemia ataturejeshea majibu mazuri,”alisema.

Alisema kuwa mlipuko wa magonjwa kama hayo umekuwepo mara kwa mara ulimwenguni na kwa nyakati tofauti wataalam wa tiba asili wamekuwa wakitumika kutafuta tiba  na wamekuwa wakifanikiwa.

“Mfano ugonjwa wa surua ulipoingia duniani watu wengi sana walikufa kwa kuwa ulikosa tiba lakini kupitia mizizi yetu ya asili, tuliweza kuokoa watu wengi kwa kujifukiza na kunywa dawa za asili, hata corona na yenyewe mwanzo ilileta taharuki kubwa sana, lakini dawa zetu za asili zilikomesha kabisa,”alisema.

Alisema mbali ya kutafuta uhakiki wa ubora wa dawa hizo kwa mkemia mkuu wa Serikali pia baada ya kupata uhakika wa tiba zake pia itakuwa ni kuziongezea thamani na hivyo kuondoa dawa ambazo ni sumu na zinazoweza kuleta athari kwa afya ya mtumiaji.

Ugonjwa wa Corona umekuwa ni tishio kubwa sana ulimwenguni lakini nchini imekuwa ni tofauti baada ya Rais Dkt Magufuli kuruhusu tiba za asili kutumika mara baada tu ya kugundulika kuingia nchini na matokeo yake yaliweza kusaidia kupungua kwa vifo na kupotea kwa ugonjwa huo.

 

 

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post