WAKAZI MKANDAMI WAONDOLEWA ADHA YA KUFUATA CHANJO UMBALI MREFU

 Na Joachim Nyambo,Mbarali.

 

HATIMAYE kilio cha wakazi wa kijiji cha Mkandami kata ya Mawindi wilayani Mbarali cha kutembea umbali mrefu kufuata huduma za chanjo kimemalizika baada ya Serikali kupeleka Jokofu katika zahanati ya kijiji chao.

 

Wakazi wa Mkandami hususani akina mama wakiwemo wajawazito walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa Kilometa 28 kufuata huduma za chanjo katika maeneo ilikokuwa ikipatikana kutokana na kile kilichokuwa kikielezwa kukosekana kwa Jokofu la kuhifadhia dawa kwaajili ya huduma hiyo kwenye zahanati ya kijiji chao.

 

Hatua hiyo ilihatarisha afya za akina mama wajawazito kwa kutembea umbali huo huku pia majukumu mengine ya kifamilia yakiwemo ya kuwaangalia watoto wadogo wakati wazazi wenzao wanapokwenda kwenye shughuli za uzalishaji mali yakiwa magumu.

 

Lakini sasa adha hiyo imeondoka baada ya jokofu kupelekwa na sasa wajawazito na watoto wanaozaliwa wanapata chanjo katika zahanati ya kijiji chao pasipo kutembea umbali mrefu hatua iliyowafanya wakazi hao kuishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao.

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,Afisa Habari wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Daudi Nyingo alisema kwa sasa wanaonufaika na upatikanaji wa chanjo jirani sit u wakazi wa kijiji cha Mkandami bali pia waishio maeneo ya jirani ndani ya kata hiyo.

 

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Kivuma Msangi alisema Jokofu lililopelekwa Mkandami ni kati ya majokofu 18 zilizonunuliwa na kusambazwa katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa na uhitaji mkubwa wilayani hapa.

 

Mjamzito Jane Kalinga ambaye pia ni mkazi wa kijiji cha Mkandami aliishukuru Serikali akisema kwa kutoa huduma ya chanjo karibu imewarahisishia akina mama kupata wasaa wa kupumzika na pia kuziangalia kwa karibu familia zao hususani kwa wale wanaokaribia kujifungua na pia wanaotoka kujifungua ambao kimsingi si vyema kutembea umbali mrefu.

 

“Chukulia kwa mfano wakati wa kilimo unakuta baba anawahi kwenda kwenye majaruba huko ya mpunga…Mama mjamzito kuna chanjo unazotakiwa kupata na wakati huo huo wewe ndiyo unapaswa kuwaandaa watoto kama wanaosoma madarasa ya awali na la kwanza.Upate muda wa kuwaandaa..utembee kufuata chanjo..bado warudi wakute chakula haujawaandalia kwakuwa ni wadogo labda wakute kiporo.Kwakweli kilichofanyika ni msaada mkubwa sana kwetu akina mama.”alisema Jane mama wa watoto wawili hadi sasa.

 

Hata hivyo katika mafaniko haya yaliyofikiwa,aliyekuwa Diwani wa kata ya Mawindi,Yusuph Mhando hana budi kushukuriwa,kutokana na jitihada alizokuwa akizifanya kupigania kupelekwa kwa jokofu la kuhifadhia dawa kwaajili ya chanjo kila alipopata nafasi ya kuchangia hoja kwenye vikao vya baraza vya Madiwani hasa vya Mapendekezo ya Bajeti.

 

Mara kadhaa Mhando alisema kwakuwa wanaume wengi wa kata yake wamekuwa wakijihusisha na shughuli za kilimo hususani cha zao la mpunga,wanawake ndiyo wamekuwa kitovu cha uangalizi wa familia hivyo wanapolazimika kutembea umbali mrefu kufuata chanjo familia zinakosa uangalizi wa karibu.

 

Mhando alisema kutembea umbari mrefu kunatokana na Zahanati iliyojengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji cha Mkandami kukosa Jokofu la kuhifadhia Chanjo licha ya kuwepo kwa miundombinu muhimu ikiwemo Nishati ya umeme.

 

“Tuliona changamoto ni kubwa ya upatikanaji wa matibabu wananchi wenyewe pasipo msaada wowote kutoka Halmashauri walichanga na kuweza kujenga zahanati.Zahanati ilifunguliwa mwaka jana lakini changamoto iliyopo mpaka leo hakuna huduma ya chanjo kwa wajawazito wala watoto.Wajawazito wanalazimika kutembea umbali mrefu mno na ni hatari kwao kwakuwa miundombine ya barabara pia hakuna..wanatembea maporini.”

 

“Suala la jokofu nimefuatilia kwa muda mrefu kwa DMO majibu ninayopewa ni yaleyale kila siku.Watu wangu wamechoshwa na adha ya kutembea muda mrefu.Wajawazito wanakosa muda wa kupumzika…wanakosa muda wa kulea familia zao na kwa huku kwetu akina mama wanapokuwa wajawazito ndiyo wanapewa nafasi ya kukaa na afamilia ili kuwezesha waume zao wakafanye shughuli za mashambani.”alisema.

 

Mara zote Mganga mkuu wa wilaya ya Mbarali Godfrrey Mwakalila alikuwa akikiri kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa jokofu kwenye zahanati ya kijiji hicho jambo alilosema linatokana na gharama ya ununuzi lakini akahidi kuwa kwakuwa kuna mgawo wa jokofu 18 zilizotarajiwa kuletwa wilayani hapa basi wakazi wa kijiji hicho watakumbukwa ahadi ambayo sasa imetekelezwa.

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Kivuma Msangi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani).(Picha na Joachim Nyambo)

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post