MONABAN - NAMWACHIA MUNGU, ATOA SADAKA KANISANI

 

NA GRACE HILLARY, ARUSHA 

MFANYABIASHARA, Dkt, Philemon Mollel maarufu kama Monaban aliyeshika nafasi ya pili kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi, (CCM) kugombea ubunge jimbo la Arusha mjini emesema mtetezi wake ni Mungu hivyo anamuachia yote.

Aliyasema hayo hana wakati yeye na familia yake walipotoa sadaka ya shukrani na kuchangia viti 10 vyenye thamani ya shilingi milioni  saba kwenye kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, usharika wa Sokon II pamoja na magunia matano ya mahindi.

Monaban alikuwa mgeni rasmi kwenye harambee ya kuchangia viti vya kanisa hilo ambapo pia ni msharika kanisani hapo.

Aliwashukuru wale wote waliomsindikiza kutoa sadaka ambapo alinukuu vipengele vya biblia vinavyoeleza ukuu wa Mungu hivyo akasema kuwa tegemeo na mtetezi wake ni Mungu hivyo ameona ni vema kutoa sadaka hiyo ya kumshukuru.

"Nimesukumwa kumshukuru Mungu kwa sababu siku zote tegemeo langu ni Mungu na najua mtetezi wangu yu hai. Baada ya mchakato wa kura za maoni nimeona nikamshukuru Mungu kwa sababu tulianza na Mungu na sasa tumefika mwisho wa kura za maoni Arusha nimeona nikamshukuru Mungu," alisema Monaban na kuongeza.

Kwa jinsi ambavyo Mungu amenilinda kuanzia mwanzo tulipoanza mchakato mpaka sasa tumemaliza salama nikaona nimwambie asante kwa sababu maandiko yanasema shukuruni kwa kila jambo, hata kwa hili nashukuru".

 "Haya ndiyo niliyokuwa nayo moyoni, mengi sina kama yatakuwepo huko baadaye tutazungumza,".

Monaban alisisitiza kuwa hana tatizo na chama chake CCM wala serikali kwani mchakato umefanyika na umemalizika na ameamua kukaa kimya.

Aidha kwenye harambee hiyo zilipatikana zaidi ya shilingi milioni 13.5 kati ya hizo fedha taslimu ni zaidi ya shilingi milioni 5.9 , ahadi shilingi milioni 1.7 na viti 10 vyenye thamani ya shilingi milioni saba.

Mwinjilisti, Philemon Loshila Mollel aliyeendesha ibada hiyo alimshukuru sana Monaban kwa kufanikisha harambee hiyo iliyowezesha  kupatikana viti 14 kati ya viti 17 vilivyohitajika kanisani hapo.

Monaban ametoa sadaka hiyo ikiwa ni siku tatu tokea Halmashauri Kuu ya CCM itangaze rasmi majina ya wagombea ubunge ambapo jimbo la Arusha mjini, Mrisho Gambo ndiye aliyeteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kwa ubunge jimbo la Arusha Mjini.

kwenye kinyang’anyiro ndani ya CCM mwaka huu, Monaban na Gambo walionekana kuchuana vikali  kwenye uchaguzi ambao ulishirikisha wagombea 91ambapo Gambo aliongoza kwa kupata kura 333 huku Monaban akiwa wa pili kwa kupata kura 68.

Dkt Philemon Mollel akiwa kanisani


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post