Wataka usafi wa watoto kunawa mikono mashuleni kuwa wa kudumu

 Na Joachim Nyambo,Mbeya.

 

WADAU ndani na nje ya jiji la Mbeya wameombwa kuendelea kuzisaidia shule jijini hapa kupata vifaa vya kutakasia mikono ili kuendeleza kampeni ya unawaji mikono si tu kwaajili ya kujikinga na ugonjwa wa Corona bali pia kuwajengea uelewa wanafunzi juu ya umuhimu wa usafi.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Mbeya,Erick Mvati amesema mahitaji ya vifaa vya kunawia mikono mashuleni ni makubwa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi ambapo kwa sasa bado kunakuwa na misongamano mashuleni kwa wanafunzi wanapotakiwa kunawa mikono.

 

Mvati aliyasema hayo alipopokea msaada wa mashine 12 za kunawia mikono na madumu 12 ya sabuni kutoka Shirika la Brac Tanzania lililokabidhi jana msaada huo ikiwa ni sehemu ya mashine 52 zilizotolewa na Shirika hilo kwa shule za msingi 52 katika mikoa mbalimbali nchini.

 

Mvati alisema licha ya maambukizi ya Corona kupungua nchini bado kuna uhitaji mkubwa wa kuchukua tahadhari ili kutoyaruhusu tena maambukizi ya ugonjwa huo na njia pekee ni kuhimiza usafi hasa katika maeneo ya watu wengi ikiwemo mashuleni.

 

“Hata kabla ya msaada huu tulikwishatoa maelekezo kuwa kila shule iwe na vifaa vya kunawia mikono kwaajili ya walimu,wanafunzi na wadau wengine wanaofika kwenye mazingira hayo.Bado tuna uhitaji mkubwa wa vifaa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi tulionao katika shule zetu.Ni muhimu wadau wakaendelea kushirikiana na Serikali kwa kuchangia ili pia tuzidi kuwapa ufahamu watoto wetu juu ya umuhimu wa usafi.Na hii sit u kwa kujikinga na Corona.” Alisisitiza Mvati

 

Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu Msingi jiji la Mbeya,Joyce Mwakifamba aliwataka wakuu wa shule za msingi zilizokabidhiwa mashine hizo kuzitunza na pale zitakapoharibika basi zifanyiwe matengenezo kwa haraka na si kwenda kuzihifadhi kama mapambo.

 

Mwakifamba aliwataka walimu kuendeleza juhudi za kuwafundisha wanafunzi kuzingatia usafi wawapo shuleni ili ujuzi huo pia waupeleke kwenye familia zao ili kuzidi kustawisha afya kwa jamii nzima.

 

Akikabidhi mashine hizo,Meneja wa Progamu ya Elimu wa Shirika la Brac Tanzania,Susan Bipa alisema nia ya Shirika hilo ni kushiriki jitihada za Serikali za kuhakikisha Corona inatokomezwa kabisa nchini na kuwaacha wananchi wakiendelea na shughuli za uzalishaji mali.

 

Alisema Shirika limeamua kuwekeza kwa watoto wa shule za msingi kwakuwa ndiko kuliko na chimbuko na msingi wa maendeleo ya kitaaluma hivyo kujenga uelewa wa usafi ni uwekezaji endelevu na wenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Meneja wa Progamu ya Elimu wa Shirika la Brac Tanzania,Susan Bipa(Kulia) akikabidhi Mashine ya kunawa mikono kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Mbeya,Erick Mvati.Shirika hilo limetoa mashine 12 na madumu 12 ya sabuni kwaajili ya shule 11 za msingi jiji la Mbeya na moja Mbeya vijijini.(Picha na Joachim Nyambo)

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post