BABU WA LOLIONDO AIBUKA NA CORONA, AIOMBA SERIKALI KUPELEKA WAGONJWA WAKAPATE KIKOMBEMchungaji Ambilikile Mwasapile kushoto akimpatia kikombe cha dawa waziri wa Ardhi, William Lukuvi (kulia) wakati huo akiwa waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na Sera
Na Mwandishi Wetu

WAKATI Dunia ikiwa kwenye taharuki kubwa ya kupambana na maradhi ya ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona baada ya kuendelea kuua maelfu ya watu duniani, Mchungaji Ambilikile Mwasapile maarufu kama Babu wa Loliondo ameibuka na kuiomba Serikali kupeleka wagonjwa wa Corona kupata kikombe cha dawa.

Akizungumza jana Aprili 22, 2020 katika mahojiano kwa njia ya simu na kituo cha redio cha Clouds Fm kupitia kipindi chake cha Jahazi, Babu wa Loliondo amesema anashangazwa na ukimya ambao Serikali imekuwa ikiufanya wakati yeye amekuwa akitoa dawa inayotibia magonjwa yote.

“Ndugu mtangazaji hii dawa ninaitoa kwa masharti ya Mungu, na imekuwa ikitibia watu wengi sana na magonjwa yote wanayoumwa, lakini tangu ugonjwa huu kuibuka nashangaa Serikali haileti watu, mimi nawaomba walete watu wachache kwa majaribio wataona maajabu ya dawa hii,” alisema.

Hata hivyo amesema hali ya ukimya ambayo imekuwa ikiendelea kwa watu kutofika kunywa dawa kujitibia maradhi ya corona umekuwa ukisababishwa na chuki ya baadhi ya watu dhidi yake ambao wamekuwa wakimuonea wivu kwa kumtangazia mambo mabaya.

Alipotakiwa kuwataja watu hao wabaya alisema muda ukifika atawaweka hadharani lakini kwa hivi sasa ataendelea kukaa kimya na kwamba bado watumiaji wa dawa yake wataendelea kutoa Tsh500 kwa kuwa bei hiyo ndio aliyooteshwa na kuagizwa kuitoza na sio vinginevyo. 

Aidha alipoelezwa kuwa ugonjwa wa Corona hauruhusu watu kusafiri kwa kuwa utasababisha maambukizi mengi na hivyo kwanini yeye asisafiri kuwapelekea dawa wagonjwa huko walipo, alisema kuwa tangu alipooteshwa na Mungu na kupewa dawa hiyo aliagizwa iwe inatolewa Loliondo katika eneo lake pekee na hivyo hatoweza kusafiri.

“kwanini  waendelee kufungia watu huko na wasiwalete hapa kupata dawa? Kama mtu anaumwa sasa ni bora afungiwe au afike kunywa dawa?,”alihoji Mchungaji Ambilikile Mwasapile.

Mchungaji Mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwasapile maarufu kama ‘Babu wa Loliondo’ anayeishi katika mji wa Samunge Loliondo, Wilayani Ngorongoro katika miaka ya karibuni amejipatia umaarufu mkubwa baada ya kutangaza kuoteshwa kupata dawa ya kutibia maradhi yote sugu ikiwemo Ukimwi, saratani na  sukari na hivyo maelfu wa watu kutoka ndani na nje ya nchi kufika kwake kupata tiba hiyo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post