WAKUU WA WILAYA ZA MOMBA NA NAKONDE WAANZA KUSAKA WANAOBADILISHA FEDHA MTAANI

Na Joachim Nyambo,Momba.

WAKUU wa wilaya za Momba mkoani Songwe,Juma Irando  na Nakonde nchini Zambia,Field Simwinga wamesema sasa dawa ya wabadilishaji fedha kiholela imewafikia na kilichobaki ni kuwatibu wasiotaka kutii agizo la Serikali.
Mkuu wa wilaya a Momba mkoani Songwe,Juma Irando(kushoto)  na Mkuu wa wilaya ya Nakonde nchini Zambia,Field Simwinga wakizindua rasmi matumizi ya Shilingi na Kwacha kwenye miji ya Tunduma na Nakonde .Nyuma yao ni Mkurugenzi wa BoT tawi la Mbeya,Ibrahim Malogoi Mkurugenzi wa Huduma za Kifedha za Benki na Mifumo ya Malipo wa  BOT,Kamanga Lazarous wakishuhudia uzinduzi huo uliofanyika katika eneo la kituo cha Huduma cha pamoja Tunduma.(Picha na Joachim Nyambo)

Wakuu hao wa wilaya wamesema baada ya Uzinduzi wa matumizi ya Shilingi na Kwacha bila kubadili kwenye miji ya mpakani ya Tunduma na Nakonde iliyo na mzunguko mkubwa wa kibiashara,wafanyabiashara wote waliokuwa wakifanya shughuli za ubadilishaji fedha kiholela ni wakati kwao kutafuta shughuli nyingine.

Walisema kwa pamoja ni muda mrefu walikuwa wakisubiri uamuzi wa Serikali na sasa kwakuwa makubaliano yamefikiwa kwa pande zote mbili ni wakati kwao kutumia vyombo vya ulinzi na usalama walivyonavyo kufanya kazi.

“Sisi tulichokuwa tunasubiri ni ruhusa tu maana ni mfumo uliokuwa na kasoro nyingi.Wananchi walikuwa wakiibiwa wakati wa kubadilisha fedha.Lakini wabadilishaji hawa hawa ndiyo waliokuwa wanatengeneza mazingira ya kupandisha na kushusha thamani za pesa zetu ili wapate faida zaidi.”

“Sasa tuna imani kuwa fedha zetu zitakuwa salama.Na kwakuwa matawi ya mabenki kwa pande zote mbili yamekwishaanza kupokea Shilingi na Kwacha tunaamini tutakuwa salama zaidi.Wafanyabiashara wetu pia sasa tumewafungulia uwanja mpana hapa mpakani kufanya biashara pasi woga wa sehemu gani sahihi atapata fedha halali na akiuza wapi atazipeleka.”alisema Irando.

Kwa upande wake Simwinga alisema“Sasa tutapita kwenye vichochoro vyote walimokuwa wanajificha wabadilishaji.Hakuna tutakayemuacha na niseme tu ni wakati kwa wananchi hasa wafanyabiashara wa pande zote mbili watupe ushirikiano ili malengo ya BoT na BoZ yaweze kufikiwa kwenye mpaka wetu.”

Naye Mkuu wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe,Jonas Mkude alisema kwakuwa changamoto zilizokuwepo kwenye mpaka wa Tunduma hazitofautiani na zilizopo kwenye mipaka ya wilaya yake na nchi jirani ikiwemo Zambia na Malawi ni muhimu BoT pia ikaelekeza mazungumzo ya namna hiyo kwenye eneo lake ili kuwaondolea usumbufu wananchi hasa wafanyabiashara.

Mkude alisema wapo wafanyabiashara ambao pia wamekuwa wakitumia mwanya wa ubadilishaji holela wa fedha mipakani kujinufaisha kwa kuwaibia wananchi wasio na uelewa wa kutosha.

Akijibu hoja hiyo Mkurugenzi wa BoT tawi la Mbeya,Ibrahim Malogoi aliahidi kulifanyia kazi suala la matumizi ya Shilingi na Kwacha ya Malawi lengo likiwa ni kuwezesha biashara rahisi mipakani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kifedha za Benki na Mifumo ya Malipo wa  BoZ,Kamanga Lazarous alisema matumizi ya Kwacha na Shilingi kwenye miji ya Tunduma na Nakonde itachoche uchumi wa wananchi wa maeneo hayo mawili na Mataifa husika.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post