RC GAMBO AZINDUA VIFURUSHI VIPYA VYA BIMA YA AFYA NHIF, AWASILISHA OMBI LA MKOPO WA X-RAY, MRI

Mwenyekiti wa mfuko wa bima ya afya ya NHIF Anne Makinda akihutubia wananchi katika viwanja vya Mbauda Jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa vifurushi vipya vya bima
Wananchi wa Arusha wakipata burudani wakati wa uzinduzi wa vifurushi vipya vya bima ya afya ktika viwanja vya Mbauda Jijini Arusha
Wanufaika wapya wa Bima ya afya wakiwa wameshika kadi zao za kupatia huduma katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akimkabidhi mmoja wa wananchi wa Arusha kadi ya bima ya afya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akikabidhi wateja wapya wa huduma ya afya kupitia vifurushi vya jipimie

Na Seif Mangwangi, Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ameuomba uongozi wa mfuko wa bima ya afya NHIF, kuangalia uwezekano wa kuupatia mkoa huo mkopo wa fedha kwa ajili ya kununulia  mashine za X-Ray, CitiScan na MRI, kwa ajili ya kurahisisha vipimo kwa wagonjwa mbalimbali wanaofika katika hospitali ya rufaa ya Mount Meru, kwa ajili ya matibabu.
Gambo, ametoa ombi hilo leo alipokuwa akizindua rasmi  vifurushi vipya vya mfuko wa bima ya afya vilivyoboreshwa katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Mbauda jijini Arusha na kusema kuwa hiyo ni aibu kwa hospital ya rufaa ya Mount Meru,kukosa mashine za kupimia magonjwa ya binadamu.
Amesema Mkoa wa Arusha ni mkubwa na hospital ya rufaa ya Mount Meru ni kongwe lakini imekuwa ikikosa mashine za kutibu magonjwa muhimu ambayo yamekuwa yakisumbua watanzania wengi.
“Ndugu Mwenyekiti wa bodi, pamoja na Mkurugenzi wako napenda kutumia nafasi hii kuwasilisha ombi rasmi la kuomba mkopo wa kununulia mashine kama za X ray, MRI na CitiScan na mimi mwenyewe nitakaa pamoja na viongozi wa hospitali kuona namna ya kuwasilisha ombi hilo mezani kwako,”amesema.
Gambo, amesema miongoni mwa faida zinazopatikana na mfuko wa bima ya afya ni pamoja na kusaidia uboreshaji wa miundo mbinu ya Zahanati,Vituo vya afya, Hospitali na pia kuhakikisha upatikanaji wa dawa  kulingana na mahitaji.
Pamoja na kupatikana kwa wataalamu wa afya, kutokana na  upungufu uliopo  maeneo ya vijijini kupitia mpango wa matumizi ya Vifurushi vya matibabu hilo litatatuliwa.
Amesema kupitia uzinduzi huo wananchi wanapata elimu kuhusu mfuko wa bima ya afya na Serikali imeweka mkakati  kuhakikisha huduma za afya zinaboreka
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa mfuko huo wa bima ya afya,Anne Makinda, amesema mfuko huo ulianzishwa mwaka 2001 ulikuwa ukilenga watumishi wa serikali tu na watu binafsi walikuwa wakichangia kwa gharama kubwa ya Shilingi Milioni 1.5 .
Amesema watumishi wa serikali walikuwa ni kikundi cha watu wachache sana  na hivyo kujikuta kundi kubwa la wananchi ambalo ni asilimia kati ya 80% hadi 90 %  wakiachwa nje ya huduma za mfuko huo.
Makinda, amesema kuwa hicho kilikuwa ni kikwazo hivyo kukafanyika maboresho na kuwezesha kuanzishwa kwa huduma ya Vifurushi vilivyoboreshwa hivyo akawaomba wananchi wawekeze ili waweze kupata huduma ya matibabu kupitia mfuko huo wa bima ya afya.
Amesema hadi kufikia mwaka huu mfuko huo umetoa mikopo ya shilingi ya bilioni 26 ambapo vituo 293 vya afya nchini vimenufaika huku mkoa wa Arusha ukiwa umeshapatiwa mkopo wa shilingi milioni 820 na kwamba malengo ya mfuko ni kuendelea kutoa  mikopo ya vifaa tiba na dawa lengo ikiwa ni kuboresha huduma za afya.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa mfuko wa bima ya afya Bernad Konga, amesema kuwa tayari wameshafanya mazungumzo na Wapagazi wa mkoa wa Arusha ili nao wajiunge kwenye mfuko huo kama yalivyo makundi mengine ya kijamii yakiwemo Bodaboda, Mama lishe na Machinga.
Amesisitiza kuwa mwananchi akiwa na Bima ana uhakika na maisha yake hivyo akahamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo wa bima ya afya ili waweze kupata huduma bora ya afya ambazo kwa sasa gharama za matibabu ni kubwa bila bima hawawezi kuzimudu. 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post