WANAWAKE 102 KUPATIWA MAFUNZO YA UDEREVA


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akifungua mafunzo ya udereva kwa wanawake 102 yanayofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo wanawake kuwa madereva mahiri wa mabasi makubwa hapa nchini.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Prof. Zacharia  Mganilwa, akitoa taarifa ya utendaji wa chuo hicho kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (hayupo pichani), kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya udereva kwa wanawake 102 yanayofanyika  jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Gillard Ngewe, akizungumza na wanafunzi  madereva wanawake 102 (hawapo pichani), watakaopatiwa mafunzo hayo katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Madereva Wanawake Bi. Martha Mimbi, akikabidhi risala kwa niaba ya washiriki  kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, mara baada ya kufungua mafunzo maalumu ya madereva hao, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akiwa katika picha ya pamoja na madereva wanawake 102  yatakayofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya madereva wanawake 102  watakaopatiwa mafunzo hayo katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), wakifurahi baada ya kufunguliwa kwa mafunzo hayo rasmi na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amefungua mafunzo ya udereva kwa wanawake 102 yatakayofanyika katika Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanawake kuwa madereva mahiri wa mabasi na hivyo kuwa chachu katika kuboresha usafiri nchini.

Akifungua mafunzo hayo ya siku arobaini na tisa yanayofadhiliwa na Benki ya Dunia, na kuratibiwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Waziri Kamwelwe, amesema kuwa mpango huo wa mafunzo umekuja wakati muafaka kwani Serikali inahitaji wataalamu wenye weledi katika miradi ambayo inaendelea kutekelezwa hapa nchini. 

“Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuijenga Nchi ya Uchumi wa Viwanda ambapo imewekeza nguvu kubwa katika kuboresha na kuimarisha miundombinu ikiwemo upanuzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha, ujenzi flyover ambayo imekamilika, ujenzi wa interchange Ubungo, pamoja na Mradi wa Mabasi yaendayo kwa Kasi (BRT) na hivyo miundombinu hii inahitaji madereva wenye ueledi katika kuilinda na kuiendeleza”, amefafanua Waziri Kamwelwe.

Ameongeza kuwa fursa hiyo imetolewa kwa wanawake kwa kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa madereva wanawake ni makini zaidi wawapo barabarani. 

“Nimefanya kazi kwa miaka mingi lakini sijawahi kuona au kusikia mwanamke amefika ofisini akiwa amelewa hivyo naamini tunaandaa wataalam wenye maadili na kazi yao”, amesema Waziri Kamwelwe. 

Waziri Kamwelwe amefafanua kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana katika kuimarisha usalama wa usafiri kwa njia ya barabara kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi yetu.

Awali akitoa taarifa Mkuu wa Chuo cha NIT, Mhandisi Prof. Zacharia M.D. Mganilwa,  amemueleza Waziri huyo kuwa Chuo kimepanga kuendelea na mafunzo hayo pamoja na kuanzisha mafunzo ya waendesha mizani ili kusaidia kupunguza changamoto za kukosa watalaamu mahiri wa masuala hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe, amesema ana imani kuwa madereva hao watakapomaliza  mafunzo hayo watakuwa waaminifu, wadilifu na wazalendo katika kulinda rasilimali ambazo watanzania kupitia kodi zao wamewekeza ili kuchangia maendeleo ya Taifa letu. 

Naye, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Taifa Fortunatus Muslim, amesema kuwa mpango huu umekuja wakati muafaka ambapo nchi inaelekea kukua kuelekea uchumi wa kati na kupanua miundombinu yake. 

Amesema kuwa ni wakati sasa wa kutoa uelewa kuwa udereva ni taaluma na sio kimbilio la wale waliokosa ajira  kwani taaluma hiyo inabeba maisha ya watu. 

Ameongeza kuwa ana imani wanawake waliochaguliwa wataleta mabadiliko makubwa kwani tafiti zinaonyesha kuwa katika ajali 110 madereva waliopoteza maisha  walikuwa madereva 109 ni wanaume na dereva mmoja ni mwanamke. 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post