WAITARA AWAONYA WATAKAOFANYA UDANGANYIFU MITIHANI YA KIDATO CHA NNE

SERIKALI imetoa onyo kwa wale wote watakaojaribu kufanya vitendo vya udanganyifu kwenye mitihani ya kidato cha nne inayoanza kesho.

Onyo hilo limetolewa leo na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Mwita Waitara alipokua akitoa salami zake za heri kwa wanafunzi zaidi ya Laki Nne wanaotarajiwa kumaliza mitihani yao ya kidato cha nne.

Mhe Waitara amewapongeza wanafunzi hao kwa uvumilivu wao kwa kipindi chote walichokua shuleni na kuwataka kufanya vizuri mitihani hiyo ili kumpa sifa Rais Dk John Magufuli kwa kutoa elimu bila malipo.

Amesema kumekuepo na vitendo vya udanganyifu kwenye vipindi vya mitihani ya Kitaifa na kuwataka wazazi na wanafunzi kutodanganyika na kushiriki vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na sheria.

" Niwapongeze Wanafunzi wote wanaotarajia kufanya mitihani hii, Sisi kama Serikali tunawatakia kila la heri, wakamtangulize Mwenyezi Mungu na kuzingatia yale yote ambayo wamefundishwa kwa miaka minne.

Lakini pia niwasihi Walimu, Wazazi na Wanafunzi kutojaribu kushiriki vitendo hivi kwa kununua mitihani kutoka kwa watu ambao wamekua wakiwalaghai kwamba wanauza mitihani. Kufanya hivyo ni kujihatarisha kwani Serikali iko makini na tukiwabaini tutawafutia mitihani,* Amesema Mhe Waitara.

Amesema tayari wameshatoa maelekezo kwa vyombo vya usalama kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaokutwa wakifanya udanganyifu huo kwani hauna tofauti yoyote na rushwa na wizi.

Waitara pia amezungumzia mafanikio ya elimu bure ambapo wanafunzi hawa wa kidato cha nne ndio zao la kwanza la elimu bure na kusema Serikali itaendelea kufanya maboresho katika sekta ya elimu na kutatua changamoto zote ambazo zipo ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira bora ya wanafunzi pamoja na walimu.

" Toka Rais atangaze elimu bila malipo hawa ndio wanafunzi wa kwanza ambao wanamaliza wakiwa wamesoma miaka minne bila malipo. Kwetu sisi ni mafanikio makubwa kuona ndoto ya Rais Magufuli ya kupambana na ujinga ikifanikiwa kwa kasi. 

Serikali imekua ikitenga zaidi ya Bilioni 23 kila mwezi kwa ajili ya elimu bure, lakini pia kuonesha mafanikio yao idadi ya wanafunzi wanaomaliza mwaka huu ni kubwa kulinganisha na ya mwaka jana. Mwaka huu wanafunzi waliosajiliwa na wanatarajiwa kufanya mitihani ni 485,000 ambapo mwaka jana waliofanya mitihani ni 427,000," Amesema Mhe Waitara.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Mwita Waitara akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma kuhusiana na mitihani ya kidato cha nne itakayoanza kesho.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post