VIGOGO WAWILI WA CHADEMA HANANG’ WAJIUNGA CCM

Mwenyekiti wa CCM Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, Mathew Darema (kushoto) akinyanyua juu mkono wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha Wilayani Hanang’ Yuda Bwanjida aliyeondoka Chadema na kujiunga CCM.
.
Mwenyekiti wa UVCCM kata ya Balang’dalalu Mkoani Manyara, Emmanuel Gamasa akipeana mkono na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha Wilayani Hanang’ Yuda Bwanjida.
………………………
 
VIGOGO wawili wa Chadema Wilayani Hanang’ wameondoka kwenye chama hicho na kujiunga na CCM ili kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais John Magufuli na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti. 
 
Vigogo hao akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la vijana la Chadema (Bavicha) wilaya ya Hanang’ Yuda Bwanjida na aliyegombea udiwani kwa Chadema mwaka 2015 kata ya Balang’dalalu Daudi Mathayo walipokewa na Mwenyekiti wa CCM wilayani Hanang’ Mathew Darema. 
 
Bwanjida akizungumza sababu za kujitoa Chadema, alisema zipo nyingi ikiwemo maendeleo mengi yanayofanywa na Rais Magufuli na usimamizi wa mkuu wa mkoa huo Mnyeti. 
Bwanjida alisema baada ya kuona viongozi wa chama chake wameangukia kwenye uanaharakati badala ya maendeleo aliamua kuachana nacho na kujiunga na CCM
“Nimejiunga na kukutana na vijana wenzangu ambao tutashirikiana kufanya kazi za kijamii kwani CCM ipo karibu na wananchi kupitia mikakati mbalimbali ya kutetea wananchi wa Taifa hili kuliko kuwa kwenye chama cha uanaharakati,” alisema. 
 
Kwa upande wake, Mathayo ambaye aligombea udiwani wa kata ya Balang’dalalu na kuangushwa na Paulo Marmo (CCM) alisema anarudi CCM ili kuwaunga mkono Rais Magufuli na Mnyeti katika kufanikisha maendeleo. 
 
Mathayo alisema yale mambo waliyokuwa wanapigia kelele wakiwa upinzani hivi sasa yanatekelezwa na Rais Magufuli hivyo haoni umuhimu wa kumpinga. 
Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) kata ya Balang’dalalu, Emmanuel Gamasa aliwapongeza viongozi hao wa upinzani kwa kuondoka Chadema na kujiunga na CCM. 
 
“Nawakaribisha viongozi hawa ambao kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 walitupa changamoto kubwa na hivi sasa tutaendelea kujenga chama chetu kwa umoja na upendo,” alisema Gamasa. 
 
Mjumbe wa mkutano mkuu wa UVCCM mkoani Manyara, Carol Gisimoy alisema viongozi hao wameona mbali kwa kuondoka Chadema na kujiunga CCM kwani wananchi wengi wanaiunga mkono. 
 
“Hakuna mtu ambaye aliwashawishi kujiunga na CCM ni wao wenyewe wameona maendeleo ya Rais Magufuli na usimamizi mzuri wa mkuu wa mkoa Mnyeti wakaona hakuna sababu ya kubaki upinzani,” alisema Gisimoy. 
 
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Hanang’ Mathew Darema alisema chama hicho kinazidi kupiga hatua na wananchi wengi zaidi wanazidi kuwaunga mkono kutokana na maendeleo yanayofanywa. 
 
“Chini ya jemedari wetu Rais Magufuli tunaendelea kutembea kifua mbele kutokana na kuendelea kuungwa mkono katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania,” alisema Darema.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post