WANANCHI 1018 WAPATIWA MSAADA KISHERIA


Na Stella Kalinga, Simiyu RS

 Msajili wa Taasisi za watoa huduma za msaada wa kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Felistas Mushi amesema  takribani wananchi 1018  wamepata huduma ya msaada wa kisheria katika maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria tangu Oktoba 21, 2019 mpaka Oktoba 25, 2019, yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.

Mushi ametoa taarifa hiyo katika Kilele cha Maadhimisho hayo, Oktoba 25, 2019 ambapo amebainisha kuwa asilimia kubwa ya matatizo ya kisheria yalihusu migogoro ya ardhi na yameshafikishwa mahakamani  na yako katika hatua mbalimbali.

Amesema huduma walizopata wananchi katika wiki ya msaada wa kisheria ni pamoja na huduma za usuluhishi, ushauri wa kisheria, kuandaa nyaraka na maelekezo ya sehemu  sahihi ya kwenda pindi wanapopata migogoro.

“Mbali na huduma kwa wananchi mafunzo yametolewa kwa makundi mbalimbali ya watumishi wa umma wapatao 1300 wakiwemo, wajumbe wa menejimenti ya sekretarieti ya mkoa, wajumbe wa kamati ya parole, wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kata na vijiji, wajumbe wa kamati ya maadili ya mahakimu, askari polisi na magereza, wajumbe wa kamati za shule na watendaji wa vijiji na kata, “ alisema Mushi.

Kwa upande wake Hakimu Mary Nyangusi akimwakilisha Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Mary Mrio, ametoa wito kwa wananchi kuandika wosia ili kupunguza migogoro ya ardhi ambayo mingi inatokea mara nyingi wanaume( baba) wanapofariki na wake(mke) na watoto kudhulumiwa haki zao.

Adam Kisinza ni Mmoja wa wananchi waliofika kupata msaada wa kisheria katika maadhimisho hayo amesema, “nashukuru nimeelewesha ninachotakiwa kufanya maana kule kwetu baba mwenye mji anapokuwa amefariki wakabaki watoto na mama, wanakuwa hawana mamlaka juu ya mali iliyoachwa maana kila mtu anataka achukue chake wakati mzee hakuacha hata  wosia”.

Akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria,Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema ni vema wizara ya katiba na sheria ikaona umuhimu wa kupeleka maadhimisho ya wiki ya msaada wa huduma za kisheria katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo, ili wananchi wapate uelewa wa masuala ya kisheria na kupata matokeo yatakayoonekana.


Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria Kitaifa mwaka 2019 yanaongozwa na Kauli Mbiu:- “Msaada wa Kisheria kwa Maendeleo Endelevu”ambapo kilele cha maadhimisho haya kimeenda sambamba na uzinduzi wa Jarida la Msaada wa Kisheria, ambalo limezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post