MWALIMU MKUU SHULE YA SEKONDARI MZINDAKAYA MKOANI RUKWA AJISALIMISHA POLISI KWA KUBAKAMkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amewaagiza wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Rukwa kuhakikisha Mkuu wa Shule ya Sekondari Mzindakaya iliyopo kata ya Kaengesa, Wilayani Sumbawanga Dastan Mlelwa anafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo baada ya kuwabaka na kuwatia mimba wanafunzi wawili wa kidato cha pili na cha tatu katika shule hiyo.

Amesema kuwa anataarifa kuwa mwalimu huyo tayari amekwishajisalimisha katika mikono ya polisi na hivyo kumtaka kamanda wa polisi mkoa, Kamanda wa TAKUKURU mkoa pamoja na Mkuu wa Usalama wa mkoa kufuatilia jambo hilo ili mwalimu huyo asitoke kwenye mikono ya polisi bali apelekwe mahakamani.

“Hili jambo hatutalifumbia macho, Mkuu wa shule kuwatafuta wanafunzi kimapenzi na mpaka kuwatia mimba, yeye kama mzazi na mwalimu haikubaliki hata kidogo, huu ni ubakaji kwasababu wale wanafunzi wa kidato cha pili na cha tatu hawana umri wa miaka 18 ni chini ya hapo, ni ubakaji,” Alisisitiza.

Katika kusisitiza suala hilo pia ameitaka kamati hiyo kufuatilia kesi ya Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mpui iliyoopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga aliyembaka na kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili na baadaye mwanafunzi huyo kuhamishwa katika shule ya Sekondari Mazwi iliyopo Manispaa ya Sumbawanga.

Katika hatua nyingine Mh. Wangabo amewaagiza wajumbe hao wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa kufuatilia kesi ya wizi wa mifugo inayomhusisha Afisa mifugo wa mji mdogo wa laela, wilayani Sumbawanga Emanuel Tluwey baada ya kukamatwa akiwa anachinja ng’ombe wa wizi kesi ambayo ilifikishwa polisi na kuonya kuwa kesi hiyo isifinyangwe finyangwe ili mwizi huoy asichukuliwe hatua.

“Lakini kuna Mazingira tata huenda kesi ikafinyangwa finyangwa na mwizi huyu asichukuliwe hatua, sasa narudisha kwa timu hii hapa, TAKUKURU yuko pale, jeshi la polisi na vyombo vingine vya usalama fuatilieni suala hili kule Laela huyu mwizi wa mifugo lazima achukuliwe hatua ya kisheria afikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo,” Alisema.

Mh. Wangabo ameyasema hayo wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika kikao maalum kilichowajumuisha wajumbe wa kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na watumishi wa seksheni ya Elimu na watumishi wa seksheni ya uchumi na uzalishaji inayojumuisha watumishi wa mifugo katika Mkoa.

Mh. Wangabo amesema kuwa nia ya kuyafanya hayo ni kupiga vita uhalifu ndani ya mkoa pamoja na ubakaji wa wanafunzi na kuonya kuwa itafika wakati kutakuwa na kura za maoni mashuleni kwa wanafunzi ili kumbaini anayewashawishi wanafunzi hao kujiingiza katika suala la mapenzi katika umri mdogo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post