MCHUNGAJI KANISA LA BAPTIST APANDISHWA KIZIMBANI AKITUHUMIWA KUJERUHI KWA VIBOKO WAUMINI WAKE KAMA SEHEMU YA MAOMBEZI NA TOBA KANISANI KWAKE

Mchungaji wa Kanisa la Baptisti Milton Wikunge akisindikizwa kwenda mahabusu baada ya kushtakiwa kwa kosa la kujeruhi waumini wake ikiwa ni katika kutekeleza ibada ya maombezi katika kanisa hilo
Na Joctan Agustino,Njombe 
MCHUNGAJI wa Kanisa la Baptisti na mkazi wa kijiji cha Mawindi, Milton Wikunge(56) pamoja na Nolbat Mbude mkazi wa Igima wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe leo oktoba 21 kujibu mashtaka ya  kujeruhi waumini watatu katika kanisa hilo.

Akisoma mastaka yanayowakabili watuhumiwa hao mwendesha mashtaka wa serikali Hapness Makungu amesema watuhumiwa wanakabiliwa na makosa matatu ya kujeruhi kinyume na Kifungu cha sheria 225 cha sheria ya kanuni ya adhabu kifungu no 16 marejeo ya 2002 ambayo waliyafanya oktoba 13 kwa watu watatu ambao wadaiwa kuwa ni waumini wa kanisa hilo ambao ni Elesi Fwami,Shahibu Mhema na Regina Lyahumi.

Watuhumiwa wote wamekana kuhusika na tuhuma hizo za kujeruhi jambo ambalo limefanya mahakama kupitia kwa hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe Iluvan Msaki kuahirisha kesi hiyo hadi octoba 31 itakapotajwa tena kwa lengo la kuendelea na uchunguzi zaidi.

APCBLOG   imezungumza na mkuu wa wilaya ya Wangingombe Comrade Ally Kassinge anakiri kutokea kwa matukio hayo ambapo amesema kwa taarifa za awali inaonyesha watuhumiwa walitoa adhabu ya viboko kwa waumini hao kwa lengo la kuwapa toba ya makosa waliyatenda na kuwasabishia majeraha makubwa kwa muumini anaetambulika kwa jina la Elisia Fwime ambaye amelazwa hospitali ya Kibena wilayani Njombe .

Kufuatia hali hiyo mkuu huyo wa wilaya anasema amejipanga kufanya ziara wilaya nzima kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kupinga vitendo vya imani potofu ikiwemo ya kanisa linalotuhumiwa kuwaadhibu waumini wao ili kutubu dhambi zao.

Watuhumiwa wote wawili ambao ni viongozi wa kanisa hilo walitiwa nguvuni na vyombo vya dola baada ya kukutwa na tuhuma za kuwaadhibu waumini wao watatu viboko na kusababisha majeraha makubwa kwa lengo la kuwapa toba jambo ambalo limepingwa vikali na serikali wilayani humo.

Katika hatua nyingine watumiwa hao wameshindwa kupata dhamana ambayo inagharimu Tsh mil 3 kutokana na wadhamini wao kukosa barua kutoka kwa mtendaji wa kata.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post