MAMA AUA MTOTO WAKE KWA KUMNYWESHA SUMU YA KUULIA WADUDU MBEYA
Na Esther Macha - Malunde 1 blog Mbeya 
JESHI la Polisi Jijini Mbeya linamshikilia mwanamke aitwaye Silvia Sande (28) Mkazi wa Nsongwi kwa tuhuma za kumuua mwanae mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili kwa kunywesha sumu ya kuulia wadudu kisha mwanamke huyo nae kunywa sumu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi Mkoani mbeya, Ulrich Matei amesema tukio hilo limetokea Septemba 16,2019 saa 4 asubuhi katika kijiji cha Nsongwi kilichopo Kata ya Ijombe, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Alisema  mtuhumiwa alikunywa sumu ya kuulia wadudu chumbani kwake kwa lengo la kujiua kisha kumnywesha sumu hiyo mtoto wake mdogo aitwaye Asifiwe Baini mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili, mkazi wa Nsongwi juu.
Hata hivyo alisema mtuhumiwa na mtoto wake baada ya tukio hilo walikimbizwa kituo cha afya Igawilo ambapo mtoto huyo alifariki. 
Kamanda Matei alisema jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kumshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano zaidi na mara baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa Mahakamani. 
Aidha alisema chanzo cha tukio kinachunguzwa.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post