Na Seif Mangwangi, Arusha
Maandalizi ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) yamekamilika jijini Arusha, huku nchi 159 kati ya 183 wanachama wa Umoja huo zikishathibitisha ushiriki wao, katika mkutano unaotarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 2,000 kutoka mabunge mbalimbali duniani.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Oktoba2, 2026 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema Tanzania imejipanga kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa mafanikio makubwa na kwa kiwango kinacholinda heshima ya taifa. Mkutano huo utafanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Spika Zungu amesema idadi kubwa ya nchi zilizothibitisha ushiriki inaonesha umuhimu wa mkutano huo na fursa ambayo Tanzania imepata ya kujitangaza kimataifa, huku akitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Amesema mkutano huo ni fursa muhimu kwa Tanzania, hususan Arusha, kuwaunganisha wageni kutoka nje na wananchi wa ndani, huku akiwataka wakazi wa Arusha kutumia fursa hiyo katika biashara, huduma za malazi, usafiri, utalii na uuzaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Spika Zungu amewataka wananchi kutumia ujio wa wageni hao kutangaza bidhaa na fursa zinazopatikana nchini, akitaja bidhaa za asili kama Tanzanite, korosho na bidhaa nyingine, huku akisisitiza umuhimu wa kuonesha ukarimu na kujenga taswira nzuri ya Tanzania kwa wageni watakaorejea katika nchi zao.
Kwa upande wake, Balozi Abdallah Posi amesema Mkutano wa 153 wa IPU ni tukio kubwa kwa Tanzania kwa kuwa ni mara ya kwanza nchi hiyo kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaowakutanisha mabunge kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Amesema Tanzania imepata nafasi ya kuonesha uwezo wake wa kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa na kuimarisha diplomasia ya kibunge.
Balozi Posi amesema wawakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mabunge Duniani na Geneva wana jukumu muhimu la kuiwakilisha na kuitangaza Tanzania katika jumuiya ya kimataifa, na kwamba ofisi hiyo ni kiungo muhimu kati ya Tanzania, Bunge na IPU katika masuala mbalimbali ya kidiplomasia.
Aidha, amesema mafanikio ya mkutano huo ni mtihani wa utayari wa Tanzania katika kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa, akisisitiza kuwa uwezo wa kufanikisha mkutano unaoshirikisha maelfu ya watu kutoka nchi mbalimbali utaongeza uzoefu na kuifanya Tanzania kuwa na uwezo wa kuandaa matukio mengine makubwa zaidi.
Balozi Posi amewataka Watanzania wote, wakiwemo viongozi, wafanyabiashara na waandishi wa habari, kushiriki kikamilifu katika kutumia fursa zinazotokana na ujio wa wageni hao, akisema wageni watakaa katika hoteli, watatembelea maeneo mbalimbali, watanunua bidhaa na kutumia huduma mbalimbali, hivyo kutoa mchango katika uchumi wa ndani.
Amesema fursa hiyo haipaswi kuishia katika diplomasia ya kibunge pekee, bali inapaswa kuzaa matokeo katika sekta ya utalii na biashara, kwani wageni watakaofika Tanzania wanaweza kuwa mabalozi wazuri wa nchi hiyo watakaporejea katika mataifa yao.
Spika Zungu amewapongeza Katibu wa Bunge na timu nzima ya maandalizi, pamoja na wahandisi, mafundi, wataalamu na watumishi wengine walioshiriki kuhakikisha miundombinu na huduma muhimu zinakamilishwa kwa ajili ya mkutano huo.
Amesema mkutano huo pia ni fursa ya kukuza utalii, kwa kuwa wageni watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali nchini na kujionea utamaduni, mazingira na huduma zinazotolewa na Tanzania.
Mkutano huo utajadili masuala mbalimbali ya kimataifa chini ya kaulimbiu inayolenga kuimarisha utawala bora na kuwezesha jamii kupitia ushirikishwaji, imani na fursa kwa wote.
Ajenda nyingine zinahusisha amani na usalama, maendeleo endelevu, haki za binadamu, wanawake na vijana pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia.
Spika Zungu amewataka waandishi wa habari kutumia nafasi yao kuutangaza mkutano huo na kuendelea kuelimisha umma kuhusu fursa zinazopatikana kupitia mkutano huo, akisisitiza kuwa mafanikio yake ni jukumu la Serikali, Bunge, sekta binafsi, wananchi na wadau wengine kwa pamoja.
Amesema ujio wa maelfu ya wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ni fursa ya Tanzania kuendelea kujenga mahusiano ya kimataifa kupitia diplomasia ya kibunge, kukuza biashara na utalii, huku Arusha ikiwa mwenyeji wa tukio hilo kubwa la kimataifa na Tanzania ikiweka historia ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani.



