Na, Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amesema Mkutano wa 46 wa Mamlaka za Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA) utawakutanisha wajumbe zaidi ya 400 kutoka mataifa mbalimbali kujadili masuala ya kodi na namna ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika nchi wanachama.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, CPA Makalla amesema mkutano huo utatoa fursa kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu na kujadili matumizi ya teknolojia katika kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, pamoja na kuangalia mbinu mbalimbali za kisasa katika usimamizi wa kodi.
Amesema Tanzania kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itapata fursa ya kujifunza teknolojia zinazotumiwa na nchi nyingine katika ukusanyaji wa kodi, huku pia ikibadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kuboresha huduma na mazingira kwa walipakodi.
Aidha, amesema mkutano huo utajadili namna ya kushirikisha na kuongeza mataifa mapya katika mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa kodi, pamoja na kuboresha uzoefu wa mlipakodi ili kuongeza ufanisi na utii wa kodi.
CPA Makalla amewakaribisha wageni wote wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo na kuwahakikishia usalama wa kutosha wakati wote wa ziara yao Arusha. Pia amewashukuru na kuipongeza TRA kwa kuaminiwa na Jumuiya ya Madola kuwa mwenyeji wa mkutano huo, akisema ni fursa muhimu kwa Tanzania.
Amesema "Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, tunawaalika wageni kupata muda wa kutembelea na kufurahia vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo mkoani Arusha.Wadau wa utalii na wamiliki wa hoteli kuweni wakarimu kwa wageni katika kipindi chote cha mkutano huo".
CPA Makalla amesema kuwa Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Dk. Deogratius Ndejembi.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mcha Hassan Mcha, amesema masuala ya teknolojia yatapewa kipaumbele katika Mkutano wa 46 wa Mamlaka za Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), kwa lengo la kuboresha mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa kodi.
Amesema mkutano huo utatoa fursa kwa nchi zinazofanya biashara za kimataifa kubadilishana utaalamu na uzoefu katika namna bora ya kusimamia shughuli za biashara zinazovuka mipaka, pamoja na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ukusanyaji wa kodi.
Vilevile Kamishna Mcha amesema washiriki watajadili kwa kina masuala ya biashara za mtandaoni na kodi katika biashara za kimataifa, hasa kutokana na mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kiuchumi duniani, ili kubaini namna mifumo ya kodi inavyoweza kuendana na maendeleo hayo.

