Mkuu wa wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amewataka madalali wanaotumika na Mahakama kukamata vitu vya watu baada ya kushindwa kulipa madeni yao kutoa taarifa katika ofisi ya Mkuu wa wilaya kabla ya kutekeleza amri waliyopewa.
Mkude ametoa agizo hilo leo Septemba 23, 2025 katika kikao chake na waandishi wa habari alipokuwa akitoa taarifa ya miaka minne ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wilaya ya Arusha chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Amesema ijapokuwa madalali hao wamekiwa wakifanya utekelezaji kwa mujibu wa sheria lakini ni vizuri ofisi yake ikaona utekelezaji huo kwaajili ya kujiridhisha na kuondoa sintofahamu inayoweza kutokea.
Hata hivyo amesema mtu akidaiwa ni lazima kulipa " dawa ya deni ni kulipa na huo ndio ukweli ambao kila aliyekopa anatakiwa kuufuata, hapa hakuna huruma," amesema
Aidha Mkude ametangaza dau la shilingi laki tano(500,000), kwa mtu atakayetoa taarifa juu ya watu wanaoharibu miundombinu ndani ya Jiji la Arusha ikiwa ni pamoja na kuiba taa za barabarani.Amesema Serikali imetumia fedha nyingi kugharamia miundo mbinu lakini watu wachache wamekuwa wakiharibi miundo mbinu hiyo kwa kuiba vifaa vinavyotumika jambo ambalo halikubaliki na kwamba kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi.
" Serikali ya Dkt Samia inatuletea maendeleo lakini wenzetu wachache wamejitokeza kutuhujumu, Kuna wanaoiba taa za barabarani na tumeanxa msako kuwakamata, nitoe wito tu Kwa watu wote kutoa taarifa hata wale wanaonunua chuma chakavu wakipelekewa chuma ambazo hawazielewi watuletee taarifa,"amesema
Amesema kwa miaka minne ya Dkt Samia madarakani Jiji la Arusha limeboreshewa mambo mengi ikiwemo sekta ya Afya, Elimu, barabara, maji na michezo ambapo jijini humo kunajengwa uwanja mkubwa wa mpira.
Mkude amesema uwanja huo ambao unajengwa katika kata ya olmot unapenda kupendezesha Jiji la Arusha Kwa kuwa pia kutajengwa miundo mbinu ya barabara za kisasa za kuingia uwanjani hapo.
Ametumia wasaa huo kuwataka watu wanaoishi karibu na uwanja huo hususani wanaoishi pembezini mwa barabara inayoelekea uwanjani kutoendeleza maeneo yao Kwa ujenzi wowote kwa kuwa Serikali inajipanga kuwalipa fidia.
" Tumeshakaa na wananchi wa eneo lile na kuwataka wasiendeleze chochote na pia nimeshawaeleza watendaji wa tanesco na auwsa kuwa ikitokea Kuna mtu anaomba huduma za maji na umeme kutowaunganishia Kwa kuwa tumeshasema tunaenda kuwalipa fidia na hawatakiwi kujenga chochote" amesema



