CRDB YAENDELEA KUPANUKA, YAFUNGUA TAWI JIPYA MPAKA WA NAMANGA

Na Seif Mangwangi, Arusha

Benki ya CRDB imefungua tawi jipya la benki hiyo katika mpaka wa Namanga, hatua inayoelezwa kulenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wa Wilaya ya Longido na kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Kenya.

Akizindua tawi hilo jipya Jana Septemba 26, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makala, amesema kuwa uwepo wa taasisi za kifedha katika maeneo ya mipakani una mchango mkubwa  kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi wa maeneo hayo sanjari na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi jirani na Tanzania.

“Katika mwaka wa fedha uliopita, mapato katika eneo hili la Namanga yameongezeka kwa asilimia 110, jambo linaloashiria kuimarika kwa shughuli za uchumi mpakani,” amesema Makala.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB,  Bonaventura Paul, amesema tawi hilo ni sehemu ya mkakati wa benki ya CRDB kufikia wananchi Kwa karibu.

“Tawi la Namanga ni sehemu ya mkakati mpana wa benki yetu wa kupeleka huduma karibu zaidi na wananchi ili kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya kifedha.”

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Tawala  wilaya ya Longido,  Rahma Kondo amesema uwepo wa benki hiyo mpakani hapo kutakuza uchumi wa wananchi wa wilaya ya Longido lakini pia kutawaondolea wananchi usumbufu wa kupata huduma za kifedha sanjari na kuwahakikishia usalama wa fedha zao.

“Benki hii imekuja wakati muafaka sana, hapa mpakani kumewepo na wafanyabiashars wengi wanaotumia fedha nyingi na wengine wamekuwa wakisafiri na fedha jambo ambalo sio salama kwao, hivi sasa watatumia benki hii kufanya mambo yao wakiwa na amani,” amesema.

Benki ya CRDB kufungua tawi hilo ni mwendelezo wa dhamira yake ya kujenga ujumuishaji wa kifedha nchini na kuwa benki ya wananchi wote mijini, vijijini, pembezoni na mpakani.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post