JAJI MKUU: UKIYATUNZA MAZINGIRA, YATAKUTUNZA.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha Joachim Tiganga akipanda mti maeneo ya Soko Kuu Jijini Arusha.

Egidia Vedasto,

Arusha.

Wananchi wamehimizwa kuendelea kutunza mazingira kwa ustawi wa afya ikiwa ni pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa maana ya gesi na umeme, kupanda miti, na kuchoma taka ngumu.

Akizungumza katika ufunguzi wa Siku ya Mazingira Duniani Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Joachim Tiganga kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania Ibrahim Mussa Juma, amesema utunzaji mazingira unakuza uchumi kwani huvutia watalii kuingia nchini kuangalia vivutio vilivyopo ambavyo ni wanyama na uoto wa asili.

Ameongeza kuwa, mazingira yasipotunzwa vizuri yanazalisha mbu wanaoeneza maleria  na matende, huku kiwango cha utupaji hovyo wa taka ngumu kwa mwaka ni takriban tani milioni saba ambazo zisipoteketezwa kwa utaratibu husababisha mafuriko kutokana na kuziba kwa mitaro.

"Ninawakumbusha wananchi kwamba kutunza mazingira ni pamoja na kutokinzana na sheria za wanyamapori, ukikamatwa na nyara za serikali adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 20, pia kila kaya mahali ilipo ipande mti mmoja ili kuimarisha uoto wa asili, kuepukana kuporomoka kwa udongo inayosababishwa na kukosekana mahali pa kujishikiza kutokana na miti kukatwa ovyo"

"Lakini pia ukataji miti bila utaratibu, uchomaji misitu, kuni na mkaa badala ya gesi na umeme vinaweza kusababisha vimbunga kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia hapa nchini na kwa mataifa mengine hali inayosababisha majanga ya vifo na upotevu wa mali" amefafanua Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga amezitaka mamlaka za mikoa, halmashauri na serikali za mitaa kushirikiana  na sekta binafsi kuendelea kupanda miti na kuweka mazingira safi , ambapo kwa mwaka inawezekana kuotesha miti milioni moja na laki tano.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amesema kuna umuhimu wa kutunza mazingira na kurudisha utamaduni kama walivyofanya mababu zetu katika utunzaji wa mazingira ili kuepuka majanga mbalimbali kama ambavyo yamekuwa yakijitokeza siku hadi siku.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa(katikati) akifanya usafi maeneo ya stendi Kuu ya Mabasi Jijini Arusha.

"Tuyatunze mazingira yetu kwa faida zetu na za vizazi vijavyo, maana tusipozingatia haya kuna hatari ya watoto wetu kutoona baadhi ya viumbe hai kama wanyama na mimea" amesema Mtahengerwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Ofisi ya Makamu wa Rais Sigsbert Kavishe amesema utaratibu wa kupanda miti uwe endelevu ili kulinda uhai wa uoto na wanyama kwa ujumla.

"Tunawahimiza wafanybiashara, asasi za kiraia na wadau wengine wa mazingira ambao ni jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti na matumizi ya nishati safi" ameeleza Kavishe.

Kwa upand wake Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini Benjamini Dotto ameeleza kuwa ni muhimu kutunza mazingira ili kuepuka ukame  na jangwa.

"Suala la usafi liwe endelevu maana linatulinda sisi wenyewe, hakuna mtu anapenda kukaa eneo chafu wala kuchafuliwa mazingira yake, tujilinde na kulinda viumbe wengine kwa kutunza mazingira" amesema Dotto.

Siku ya mazingira Duniani imeadhimishwa leo mikoa yote nchini ikiambatana na shughuli za upandaji miti na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali, ambapo kilele chake kitafanyika tarehe 5 Juni Jijini Dodoma huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mipango.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post