DC ARUSHA: KLINIKI YA KERO AWAMU YA PILI KUANZIA MEI 22-24 MWAKA HUU

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa

Egidia Vedasto

Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa anatarajia kuzindua kliniki ya kusikikiza kero za wananchi kuanzia Mei 22 hadi 24 mwaka huu.

Kliniki hii ni muendelezo baada ya kufanyika nyingine ya awamu ya kwanza mwezi Machi mwaka huu.

Akizungumza na Mwandishi wa APC Online Ofisini kwake amewataka wananchi wote wilayani humo kufika katika viunga vya ofisi yake ili kupata mwarobaini wa changamoto zao.

Aidha amesema kuwa, mfululizo wa kuzikiliza kero umekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda kuwaagiza Wakuu wote wa Wilaya ya Arusha kusikiliza kero za wananchi ambazo zimekuwa sugu na kutotatuliwa kwa muda mrefu.

" Tutaanza kusikiliza kero hizo kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa tisa mchana kwa siku zote tatu, hivyo nawasihi wananchi wote wa Wilaya hii kuzingatia muda huo ambao naamini utatuzi na ufumbuzi wa kero utapatikana" amesema Mtahengerwa.

Kwa Upande wake mmoja wa waendesha bodaboda maeneo ya kilombero Said Hamza, amesema utaratibu huu ni mhimu na umesaidia wakazi wa arusha kwani migogoro mingi imetatuliwa na wananchi wanatoa ushuhuda.

"Ninachoweza kusema isiwe mwisho wa kusikiliza kero, iwe muendelezo ili kila mwenye changamoto asikilizwe na kupatiwa majibu, maana huko maofisini hata ukienda na shida watumishi wanajifanyaga wako bize sana na kutojali, lakini kwa staili hii naamini Arusha itakuwa shwari" ameeleza Hamza.

Hatahivyo Mzee wa mila wa kabila la Kimasai anayeishi kata ya Kisongo Zakayo Mollel ameishukuru serikali kwa usikilizaji wa kero na kuomba uendelee.

" Mimi ni mzee wa miaka sabini lakini kuna migogoro ya ardhi ambayo nimedai haki kwa miaka mingi, lakini kutokana na hizi kliniki za kero zimefanya haki yangu ikapatikana, ninaipongeza serikali kwa kazi nzuri" amefafanua Mzee Mollel.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post